Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kithure Kindiki, ametoa amri ya kuwaua wahalifu wanaolenga kuwashambulia maafisa usalama au kambi za usalama.
Hayo ameyabainisha wakati wa uzinduzi wa kambi ya kijeshi ya huduma jumuishi (GSU) katika jimbo la Tiaty kaunti ya Baringo.
"Yeyote anayewashambulia wale waliopewa jukumu la kulinda Wakenya atashughulikiwa kikatili,''Amesema Kindiki
Waziri huyo pia amesisitiza nia ya serikali katika kumaliza hali ya kutokuwepo kwa usalama katika eneo hilo, na kuongeza kwamba Serikali ya Kenya imepanga kuanzisha kambi kadhaa ili kudhibiti uhalifu wa mara kwa mara katika eneo hilo.
Maagizo hayo yametolewa siku chache baada ya majambazi wenye silaha kuwaua watu watatu katika shambulio huko Baragoi, Kaunti ya Samburu.