Dar es Salaam. Waziri asiyekuwa na wizara maalum nchini Kenya, Raphael Tuju amejeruhiwa baada ya kupata ajali ya gari.
Waziri huyo ambaye pia ni katibu mkuu wa chama tawala cha Jubilee alipata ajali leo Jumatano Februari 12 akiwa njiani kuhudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi yanayofanyika katika Kijiji cha Kabarak, Nakuru.
Taarifa zinasema kuwa baada ya Tuju kupata ajali alipelekwa katika Hospitali ya Kijabe nchini Kenya.
Inaelezwa kuwa waziri huyo alipata maumivu ya kifua na taratibu zinafanyika ili ahamishiwe kwenye Hospitali ya Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi.
Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Prado. Wengine waliojeruhiwa ni pamoja na dereva na mlinzi wake ambao walitibiwa na kuruhusiwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Nation ya Kenya, gari ya waziri huyo iligongana na gari ya abiria maarufu matatu katika eneo la Magina katika barabara kuu ya Nairobi- Nakuru.
Pia Soma
- WHO yapata jina rasmi la ugonjwa wa corona
- NEC wazungumzia ratiba feki uchaguzi mkuu 2020
- Moto waacha simanzi soko la Makoroboi jijini Mwanza
Rais Moi ambaye alifariki dunia Jumanne iliyopita anazikwa leo nyumbani kwake katika Kijiji cha Kabarak Kaunti ya Nakuru.