Mamlaka ya Uganda inamshikilia aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Usalama wa Ndani wa Kenya Stephen Tarus kwa tuhuma za kuingiza dhahabu nchini humo kwa kutumia nyaraka ghushi.
Bw Tarus alikamatwa wiki jana na kufikishwa mbele ya mahakama ya Uganda ya kukabiliana na ufisadi siku ya Jumatano kwa kughushi nyaraka za mauzo ya nje, Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) ilisema.
Nyaraka za biashara haramu zilisababisha hasara kubwa ya kifedha kwa serikali ya Uganda, URA iliongeza.
Alishtakiwa kwa kughushi nyaraka za mauzo ya nje kwa kilo 13 za dhahabu yenye thamani ya $30,000 (£24,000).
Dhahabu hiyo ilitumwa Dubai katika eneo linaloshukiwa kuwa la magendo, kulingana na URA.
Bw Tarus anazuiliwa katika gereza la Luzira hadi Januari 18, akisubiri uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.
Tarus mwenye umri wa miaka 57 aliwahi kuwa waziri msaidizi chini ya hayati Rais Mwai Kibaki na kama balozi wa Kenya nchini Australia kati ya 2009 na 2012.
Pia aliwahi kuwa mbunge kati ya 2003 na 2007.