Waziri mkuu wa Japan ameonana na Rais Macky Sall wa Senegal na kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Tokyo inaunga Umoja wa Afrika AU kuwa mwanachama wa kudumu wa G-20 ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya Japan ya kujikurubisha zaidi na kutafuta ushawishi ndani ya nchi za Afrika.
Shirika la habari la Kyodo News la Japan limemnukuu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Fumio Kishida akisema katika mazungumzo yake hayo na Rais Macky Sall wa Senegal mjini Tokyo kwamba, kwa kuzingatia kuongezeka nafasi ya nchi za Afrika katika jumuiya ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni, Japan ina nia ya kuimarisha uhusiano na Afrika kwenye nyuga zote na inaunga mkono nchi za Afrika kuwa wanachama wa G20 kupitia AU.
Rais Sall, ambaye pia ni mwenyekiti wa hivi sasa Umoja wa Afrika AU ameelezea kufurahishwa na pendekezo hilo la Waziri Mkuu wa Japan na kusema kuwa lina manufaa kwa nchi zote za Afrika. Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja katika miradi ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia nchini Senegal.
Waziri Mkuu wa Japan ameahidi kuwa, Tokyo itatoa hadi yen bilioni 10 (dola milioni 72.8) katika mikopo yenye riba nafuu kwa sekta ya elimu nchini Senegal na hadi yen bilioni 15.42 (dola milioni 112.3) kama msaada wa kuchangia ruzuku ya serikali ya Senegal katika sekta ya uvuvi.
Viongozi wa Afrika wamekuwa wakilalamikia kutengwa na kutojumuishwa bara hilo katika taasisi muhimu duniani kama G20 na kutopewa uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya mchango wao mkubwa katika ustawi wa uchumi wa dunia.
Ijapokuwa nchi za Magharibi siku zote zinaliangalia bara la Afrika kwa jicho la kikoloni lakini mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama yaliyotokea ulimwenguni yamezifanya nchi za Afrika kuwa na umuhimu mkubwa na makhsusi katika mfumo wa kimataifa