- Msimamizi huyo wa mtihani katika kaunti ya Migori alibambwa akisambaza karatasi za mitihani kabla ya wakati wa kuuandika kuwadia
- Magoha alitoa onyo kali kwa watahiniwa akisema watachukuliwa hatua za kisheria wakihusishwa na udanganyifu
- Mtihani huo wa kitaifa ulianza Ijumaa, Machi 26, baada ya KCPE
Waziri wa Elimu George Magoha siku ya Jumanne, Machi 30, alitangaza kwamba msimamizi wa mtihani katika kaunti ya Migori alibambwa akisambaza karatasi za mitihani kabla ya wakati wa kuuandika kuwadia
Magoha alitoa onyo kali kwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa kidato cha nne(KCSE) dhidi ya kushiriki udanganyifu katika mtihani huo unaoendelea.
Kwa mujibu wa Taifa Leo, Waziri huyo pia aliwaonya walimu na wasimamizi wa mitihani kutojihusisha na udanganyifu akisema watachukuliwa hatua za kisheria.
“Leo Jumanne, tumekamata msimamizi katika shule moja eneo la Migori akisambaza karatasi za mitihani kabla ya wakati wa kuuandika kuwadia. Atafikishwa kortini afunguliwe mashtaka.
“Watahiniwa watakaojaribu kutumia mbinu za hila kupita mtihani, tutawaadhibu kisheria. Hatutasaza mhusika yeyote,” alisema waziri huyo.
Katika taarifa nyingine inayofungamana na KCSE, watahiniwa sita wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Bungoma Baptist walifukuzwa shuleni baada ya kununua biskuti kutoka kwa mchuuzi kinyume na sheria za shule hiyo.
Sita hao walifukuzwa Jumamosi, Machi 27, siku moja baada ya mtihani wa kitaifa kuanza rasmi mnamo Ijumaa, Machi 26.
Wazazi walidai kuwa watahiniwa hao waliagizwa kutokea nyumbani kila siku kufanya mtihani na pia walichapwa, kunyimwa chakula na kulazimishwa kulala katika chumba cha walimu kabla ya kutumwa nyumbani.
Na sasa wanamtaka Waziri wa Elimu George Magoha kuingilia kati suala hilo ili wanafunzi hao waruhusiwe kufanya mtihani wakiwa shuleni.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.