Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wapatwa hofu tupu kidato cha kwanza

Maabara Wanafunzi Wazazi wapatwa hofu tupu kidato cha kwanza

Mon, 16 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazazi, walimu na watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa shule ya msingi (KCPE) 2022, wanasubiri roho mikononi matokeo ya uteuzi wa nafasi za kidato cha kwanza kabla ya masomo ya mwaka huu kuanza Januari 23.

Watahiniwa 1,233,852 walishiriki katika mitihani hiyo ya kitaifa ya mwaka jana na wote wamehitimu kujiunga na kidato cha kwanza, kuambatana na sera ya serikali kwamba wanafunzi wote sharti wajiunge na shule ya upili.

Kati ya watahiniwa hao, 620,965 (asilimia 50.32) walikuwa wavulana, ilhali 612,887 walikuwa wasichana.

Katika shughuli hiyo, wanafunzi kumi bora (wavulana watano na wasichana watano) kutoka kila kaunti ndogo nchini, watajiunga na shule za kitaifa walizochagua.

Kuna kaunti ndogo 290 nchini, kumaanisha kwamba wanafunzi 2,900 watapata fursa ya kujiunga na shule walizojichagulia. Serikali haijabadilisha vigezo vya uchaguzi wa wanafunzi ambavyo hasa vinaangazia ustahilifu, usawa na chaguo la mwanafunzi.

“Shughuli za kuchagua wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza zinafanywa na kompyuta. Hiyo ndiyo mbinu tuliyotumia,” asema Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu.

Kuna wazazi ambao tayari wameonyesha wasiwasi wao wakihoji kwamba utaratibu huu utawapendelea wanafunzi katika shule za umma.

Mwenyekiti wa kifaifa wa chama cha wazazi Bw Silas Obuhatsa alitoa mwito kwa uwazi na uwajibikaji kuzingatiwa wakati wa shughuli hiyo. Alisema kwamba shughuli za miaka ya awali zilionekana kutowafaa wanafunzi kutoka shule za msingi za kibinafsi.

“Tunaomba haki katika shughuli za kuchagua wanafunzi zinazoendeshwa na Wizara ya Elimu pekee. Wanafunzi wanapaswa kupewa fursa ya kujiunga na shule walizochagua, na wazazi wanafaa kuhusishwa katika shughuli hizi katika siku zijazo,” Bw Obuhatsa alisema.

Aliiomba serikali kuhakikisha kwamba watoto katika shule binafsi pia wanapata nafasi katika shule kuu za kitaifa.

“Watoto wote wako sawa na hivyo mtoto yeyote anayepata alama zinazomruhusu kujiunga na shule ya kitaifa, hapaswi kunyimwa nafasi hiyo,” aliongeza, huku akiiomba Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba wanafunzi hawapelekwi katika shule ambazo hawakuchagua.

“Hili limekuwa suala tata kila wakati wa shughuli za kuchagua wanafunzi unapofika, lakini mara hii tunahitaji kutenda haki. Wapeleke wanafunzi katika shule ambazo wamehitimu kujiunga nazo,” alisema.

Shughuli hii ambayo inaendeshwa na Wizara ya Elimu, Baraza la kitaifa la mitihani nchini (KNEC) na Halmashauri ya Teknolojia habari na mawasiliano (TEHAMA), inatarajiwa kukamilika wikendi ijayo na matokeo kutolewa Jumatatu au Jumanne, ili kuwapa wazazi nafasi ya wazazi kuandaa wanao kujiunga na kidato cha kwanza.

Katibu mkuu wa Muungano wa walimu wa shule za sekondari na taasisi za masomo (Kuppet), Bw Akelo Misori, ameiomba wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba shughuli hizi zinatekelezwa kwa haki, huku akisitiza kwamba chaguo la wanafunzi linapaswa kuheshimiwa.Nchini kote kuna shule 112 za kitaifa, shule 776 kuu za kaunti, shule 1,301 za kaunti, shule 6,297 za kaunti ndogo na shule 1,301 za kibinafsi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live