Ibada ya kanisa katika mtaa wa Kawangware jijini Nairobi ilikatishwa ghafla baada ya wuamini wenye ghadhabu kuzua rabsha kufuatia ombi la mchungaji wao kuwataka wamchangie pesa za kununua gari la kifahari aina ya Prado TX.
Tukio hilo lililofanyika Jumapili tarehe 10 Desemba katika kanisa moja mtaani humo na kuzua mjadala mkali pindi tu baada ya kupenyeza katika mitandao ya kijamii.
Washiriki waliokuwa na hasira waliimba na kushikilia mabango nje ya kanisa yaliyosema ‘Askofu lazima aende.’
Askofu huyo alielezea masikitiko yake kwa waumini kwa kushindwa kuchangisha pesa za kumnunulia Prado.
Pia alieleza kuwa aliona aibu alipokutana na Wachungaji wengine waliokuwa wakiendesha magari bora kuliko yeye.
"Alikuwa amesema kwamba alihitaji gari kwa sababu mara nyingi aliaibishwa wakati wa mikutano wakati maaskofu wengine walikuwa na magari ya kifahari," James Gichuhi, meneja wa fedha wa kanisa hilo alifichua kwa vyombo vya habari.
Licha ya wanachama hao kueleza matatizo yao ya kifedha, askofu huyo aliendelea kusema kuwa wamekataa kumnunulia gari hilo baada ya kuchangisha mamilioni ya pesa za kununua basi la shule.
Pia walidai kuwa Askofu huyo mara moja baada ya nyingine angeshambulia viongozi wa kanisa katika mahubiri yake.
Mmoja wao ambaye alikuwa mkalimani alieleza ugumu wake katika kutafsiri kwani alisema kauli nyingi zilielekezwa kwa baadhi ya watu wa kanisa.