Watu wasiopungua tisa wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika matukio mawili tofauti ya ufyatuaji risasi nchini Afrika Kusini.
Kamishna wa kieneo wa Polisi ya Afrika Kusini, Elias Mawela alisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, watu wanne waliuawa na wengine wawili walijeruhiwa katika tukio la kwanza lililotokea usiku wa kuamkia jana katika kitongoji duni cha Thembelihle, kusini mwa jiji la Johannesburg.
Naye Kanali Andre Traut, afisa mwandamizi wa Polisi ya Afrika Kusini amesema wameanzisha uchunguzi wa mauaji ya watu watatu kwa kupigwa risasi katika mji wa Khayelitsha, mkoani Western Cape Jumamosi usiku.
Habari zaidi zinasema kuwa, mtu wa nne aliuawa kwa risasi usiku huohuo katika tukio ambalo halihusiana na hilo la mauaji ya watu watatu katika mji wa Khayelitsha.
Matukio hayo ya ufyatuaji risasi yamejiri wiki moja baada watu 21 kuuawa kwa kupigwa risasi na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika matukio matatu tofauti ya ufyatuaji risasi yaliyotokea kwenye vilabu na kumbi za starehe nchini Afrika Kusini.
Watu zaidi ya 20,000 huuawa kila mwaka nchini Afrika Kusini katika matukio mbalimbali ya uhalifu, taifa lenye jamii ya watu milioni 60.