Watu sita waliuawa Jumatano nchini Kenya katika mapambano kati ya polisi na waandamanaji walioshiriki maandamano ya upinzani yaliyopigwa marufuku, maafisa na polisi wameliambia shirika la habari la AFP.
Baada ya ghasia hizo za Jumatano, waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki alitoa onyo akisema kwamba serikali haitavumilia tena.
“Watu wamepoteza maisha, maafisa kadhaa wa usalama na raia wamejeruhiwa vibaya na hasara kubwa kwa uchumi wa nchi imetokea,” alisema katika taarifa ya kulaani “ghasia zilizotokea katika maeneo kadhaa ya nchi, uporaji na uharibifu wa mali za watu binafsi na umma”.
Mapema Jumatano, polisi waliwafyatulia waandamanaji gesi ya kutoa machozi ndani na karibu na mji wa Nairobi, huku vifo vya watu watano kati ya hao sita vikiripotiwa katika miji ya Mlolongo na Kitengela nje kidogo ya mji mkuu wa Nairobi.
Gesi ya kutoa machozi ilitumiwa pia kutawanya umati wa watu walioshambulia barabara kuu inayounganisha Nairobi na mji wa bandari wa Mombasa, huku kifo cha mtu mmoja kikiripotiwa katika mji wa Emali, ulio kando ya barabara hiyo.
Afisa mmoja wa polisi ameiambia AFP “kuna vifo vya watu watatu Mlolongo, ambapo kundi la waandamanaji walikuwa wamefunga barabara ili kuandamana, na pia kuna wengine wawili waliouawa Kitengela na mmoja Emali.”
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, akiendelea na kampeni ya kuipinga serikali, aliitisha maandamano ya kupinga sheria ya fedha 2023 ambayo imesababisha bei ya mafuta kupanda, na kuongeza matatizo kwa Wakenya maskini.