Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu saba wahofiwa kufariki baada ya kuvuka mto uliofurika Kenya

Watu Saba Wahofiwa Kufariki Baada Ya Kuvuka Mto Uliofurika Kenya Watu saba wahofiwa kufariki baada ya kuvuka mto uliofurika Kenya

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: Bbc

Takriban watu saba wanahofiwa kufariki baada ya kusombwa na mto uliofurika kusini-mashariki mwa Kenya.

Chifu wa eneo hilo amesema walikuwa wameketi kwenye gogo katikati ya mto walipokuwa wakijaribu kuvuka maji yalipozidi na kuwachukua.

Kundi hilo lilikuwa likirejea makwao katika Kaunti ya Makueni baada ya kukutana na Mke wa Rais Rachel Ruto jijini Nairobi.

Kenya, pamoja na nchi jirani za Somalia na Ethiopia, zinakabiliwa na mafuriko makubwa zaidi katika historia ya hivi majuzi.

Walioshuhudia waliambia vyombo vya habari kuwa watu kadhaa walikuwa wamekwama baada ya Mto Muooni kujaa maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa saa kadhaa, lakini kundi hilo liliamua kujaribu kuuvuka hata hivyo Alhamisi jioni.

"Walikuwa wameketi juu ya gogo lililokuwa likielea katikati ya mto baada ya kuzidiwa na maji yaliyokuwa yakivuma walipokuwa wakijaribu kuvuka," chifu wa eneo hilo Norman Musyoki aliambia gazeti la kibinafsi la Daily Nation.

"Kujaa ghafla kwa mto kuliwasomba huku umati wa mashahidi ukitazama bila kujua cha kufanya."

Alisema kuwa mamlaka ilikuwa ikijaribu kubaini idadi kamili katika kundi hilo, lakini mashahidi wanasema takriban watu saba wamesombwa.

Juhudi za uokoaji za serikali za mitaa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya zinaendelea kwa sasa.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na mafuriko - ambayo yanatokana na hali ya hewa ya El NiƱo - yameua takriban watu 71 na kuwafanya zaidi ya 150,000 kuyahama makazi yao nchini Kenya, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya.

Kaunti 33 kati ya 47 zimeathiriwa, lakini Makueni ni mojawapo ya zilizoathirika zaidi.

Licha ya maafa yalioenea, Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua Jumatano alisema kuwa serikali ya kitaifa haitafadhili juhudi za kukabiliana na mafuriko.

Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 130 nchini Kenya, Ethiopia na Somalia, kwa mujibu wa shirika la misaada la Oxfam.

Chanzo: Bbc