Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu milioni nne Afrika wafa kila mwaka kisa nishati chafu

MAITI YAPOTEA Watu milioni nne Afrika wafa kila mwaka kisa nishati chafu

Mon, 29 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk.Selemeni Jafo amesema takwimu zinaonesha watu milioni nne Afrika wanapoteza maisha kila mwaka kwasababu ya kutumia nishati chafu ikiwemo ya kuni na mkaa.

Hivyo, amesema ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha kampeni ya kuhamasisha nishati safi Afrika inapaswa kuungwa mkono na watu wote.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi 1,500 na majiko kwa wananchi wa Jiji la Arusha wakiwemo wajasiriamali.

Dk. Jafo amesema matumizi ya kuni na mkaa nchini yanasababisha hekta 46,242 za miti kupotea kila mwaka kwasababu wananchi wanakata kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Dk.Jafo amesema matumizi ya nishati safi inakwenda kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kampeni ya kuhamasisha nishati safi.

“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amekuwa na dhamira njema na ndiyo maana amekuja na kampeni ya nishati safi ya kupikia. Haya ni mapenzi yake na kwasababu tunafahamu nishati chafu inamadhara makubwa katika mazingira,” amesema Jafo.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa kinamama na wasichana kwa asilimia kubwa wanatumia wastani wa saa 20 kwa wiki kwa ajili ya kutafuta kuni na mkaa.

“Leo hii ukiona nchi imejipanga katika nishati safi ya kupikia ni jambo la msingi lenye kutia matumani. Watafiti wanatuambia kitendo cha kutumia nishati safi ya kupikia kwa akina mama wajazito kunasaidia kurekebisha presha ya mama mjazito,” amesema Dk. Jafo.

Amesema nishati safi inasaidia mama mjazito kupata mtoto mwenye uzito unaokubalika anapozaliwa, hivyo kuna faida nyingi kutumia nishati safi ya kupikia.

“Nina fahamu mpaka leo hii Oryx wameshatoa mitungi ya gesi 32,000 kwa ajili ya jamii na wameshatumia Sh.bilioni 2.7 lakini bado wameendelea kuendelea na kampeni hiyo kwa kutoa mitungi kwa jamii,” amesema Dk. Jafo.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia kuhamasisha nishati safi ya kupikia wameona ni vema kuendelea kuyagusa makundi mbalimbali katika jimbo hilo.

Amesema kabla ya kugawa mitungi hiyo 1,500 ya Oryx kwa wakazi wa Arusha Mjini, tayari ameshagawa pia mitungi 1,400 kwa wajasiriamali, huku akisisitiza wataendelea na kuyafikia makundi yote yakiwemo ya watoto wanaolelewa vituo vya ya watoto yatima.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya gesi ya Oryx, Benoite Araman alisema Tanzania, wananchi 33,000 wanapoteza maisha kila mwaka kwa kuvuta moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na kuni.

Amesema kupika kwa kutumia gesi ya Oryx huzuia ukataji miti, kwa hiyo husaidia kulinda mazingira, huku akieleza pia kutumia gesi ya Oryx huzuia wanawake kutumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa msituni.

Amesema: "Kupika kwa kutumia gesi ya Oryx ni kupika kwa haraka na kwa ufanisi zaidi; kwa hiyo, wanawake wataanda chakula kwa wakati na wanaume hawatalalamika juu ya kuchelewa kwa chakula kinachosababisha mizogo”.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live