Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema zaidi ya watu milioni 780 wanateseka kwa njaa kote ulimwenguni, lakini wakati huo huo karibu theluthi moja ya chakula ulimwenguni kinaharibiwa au kupotea.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameyasema hayo kwenye mkutano wa viongozi kuhusu Mifumo ya Upatikanaji wa Chakula huko Roma, Italia jana Jumatatu akisema bado inastaajabisha kuwa katika dunia yenye utajiri bado kuna watu hawana chakula au wanakufa njaa.
Amesema mifumo ya chakula duniani kuanzia shambani hadi mezani imesambaratika na kusababisha zaidi ya watu bilioni tatu wakose mlo wenye lishe na zaidi ya milioni 780 hawana chakula.
Ameieleza hadhira ya mkutano huo kuwa licha ya changamoto kwenye mifumo ya chakula, kuna nuru katika kuiboresha kwani tayari nchi zinaitikia wito wa mwaka 2021 wa kuboresha mifumo ya chakula.
Nchi 100 zimewasilisha ripoti zao za jinsi ambavyo zinatunga sera na kujumuisha katika mipango ya kitaifa hatua za kuimarisha mifumo hiyo.
Hata hivyo ili dunia iwe na mifumo bora na endelevu ya kuzalisha na kusambaza chakula na itakayofanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, Katibu Mkuu amependekeza mambo makuu matatu.
Mosi; uwekezaji wa kiwango kikubwa kwenye mifumo ya chakula endelevu, yenye uwiano, afya na mnepo. Pili; serikali na sekta binafsi zishirikiane kujenga mifumo ya chakula itakayojali watu badala ya faida na tatu; kuhakikisha mifumo ya chakula haiharibu mazingira ya sayari dunia.
Kuanzia tarehe 24 hadi 26 mwezi huu wa Julai, mkutano huu wa pili wa viongozi kuhusu mifumo ya chakula, unafanya tathmini ya kilichofanyika tangu mkutano wa kwanza mwaka 2021.
Zaidi ya washiriki 2,000 kutoka nchi zaidi ya 160 wanashiriki kuangalia mafanikio na changamoto za kufikia mifumo endelevu ya chakula duniani,
Mada zinazomulikwa ni pamoja na upotevu wa chakula, mabadiliko ya tabianchi, lishe bora, sayansi na teknolojia, ufahamu wa watu wa jamii ya asili na usafirishaji