Mzozo huo umewalazimu takriban watu milioni 3.5 kukimbia makazi yao wakiwemo 844,000 ambao wamekwenda nchi jirani kutafuta usalama kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya makundi 30 ya haki za binaadam nchini Sudan na taasisi za kitaaluma zilishutumu Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi (RSF) kwa kutekeleza ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia katika jimbo la Darfur nchini Sudan na kwingineko.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumamosi mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yalitaka uchunguzi wa haraka kuhusu ukiukaji huo ufanyike na suala hilo lipelekwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na VOA Nafisa Hajar naibu mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Darfur anasema wameandika taarifa kuhusu mfululizo wa vitendo vya ukiukwaji na mashambulizi ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki, mauaji ya kikabila na kuhamishwa kwenye makazi yao kwa nguvu, ambayo anasema vinapelekea uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu,
Anasema kutokana na kwamba mfumo wa mahakama wa Sudan sasa umekwama kutokana na vita vinavyoendelea jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua kuwafikisha wahusika mahakamani.
Hajar anasema hivi sasa mashambulizi ya anga yanaendelea kwenye majengo ya raia, raia nao wanahamishwa kwa nguvu kutoka kwenye makazi yao wanawake wanabakwa. Kwa hivyo anasema tunaamini kwamba ukatili huu wote unapaswa kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita.
Julai 13, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu –ICC Karim Khan alitangaza kufunguliwa kwa uchunguzi mpya kuhusu tuhuma za uhalifu wa kivita katika mazingira ya vita vya Sudan hususan katika mji wa El Geneina katika jimbo la Darfur Magharibi.
Hajar anasema nia ya ombi lao ni kuwasaidia waathirika na kuzuia kuendelea kwa kutokuadhibiwa kwa wahusika wanaodaiwa kuhusika.
Anasema wote jeshi na RSF wanastahili kuchunguzwa
Mwanasheria wa Sudan Abdul Basit Al Haj alikosoa Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan kwa kushindwa kuwalinda raia huko El Geneina wakati wa mashambulizi ya RSF katika mji huo na kwingineko nchini Sudan.
Akizungumza na VOA, Al Haj anasema RSF imekuwa ikishambulia hospitali, kuzikalia kimabavu, wakiwalenga madaktari mjini Khartoum na kufanya mauaji ya halaiki na mauaji ya kikabila kwa makundi yasiyo ya Waarabu, hususan kabila la Masalit katika jimbo la Darfur Magharibi.
Msemaji wa Jeshi la Sudan Nabeel Abdallah alilitenga jeshi lake na ukatili huu akisema yote yalifanywa na RSF.
Waliteka nyumba za raia huko Khartoum kwa nguvu na kuzigeuza kuwa kambi za kijeshi, Nabeel aliiambia VOA.
VOA ilimtafuta mshauri maalum wa kamanda wa RSF kwa masuala ya kigeni Ibrahim Mukhayer kwa maoni lakini hakujibu.
Vita vilianza kati ya jeshi na vikosi vya RSF Aprili 15. Mzozo huo tangu wakati huo umewalazimu takriban watu milioni 3.5 kukimbia makazi yao wakiwemo 844,000 ambao wamekwenda nchi jirani kutafuta usalama kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.