Watu 76 wamefariki dunia nchini Nigeria na 15 wameokolewa baada ya boti kuzama kusini mashariki katika jimbo la Anambra, Nigeria, eneo lililokumbwa na mafuriko makubwa.
Boti hiyo ilizama siku ya Ijumaa huko Umunnankwo katika Manispaa ya Ogbaru, iliyoko kwenye Mto Niger na haijabainika ni watu wangapi walikuemo katika boti hiyo.
Afisa wa huduma za dharura za serikali ya Nigeria, Chukwudi Onyejekwe amesema “Tumeokoa watu 15 na wengine wengi hawajulikani walipo, hadi sasa hakuna maiti iliyopatikana na kwamba shughuli za utafutaji zinaendelea.”
Maeneo mengi ya Nigeria yameathiriwa na mafuriko tangu kuanza kwa msimu wa mvua ambayo yamesababisha vifo vya watu 300 na wengine 100,000 kukosa makazi, hata hivyo maeneo makubwa yanayolimwa yameharibiwa na hivyo kuzua hofu ya kuongezeka kwa uhaba wa chakula nchini.
Rais Muhammadu Buhari amesema kwamba takriban watu 85 walikuwa wamepanda boti hiyo siku ya Ijumaa wakati mawimbi makali ya Mto Niger yalisababisha kuzama kwake.
Maafisa wa serikali wanasema boti hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 100, injini yake ilishindwa kuhimili makali ya mawimbi ya bahari.
Hata hivyo serikali ilisema kuwa jeshi tayari limetumwa eneo hilo la mkasa kusaidia katika shughuli za uokozi lakini huduma za dharura zilisema kuwa kupanda kwa kiwango cha maji kunatatiza juhudi za uokoaji.
Ajali za boti hutokea kila mara nchini Nigeria kwa sababu ya kubeba abiria kupita kiasi, mwendo wa kasi, ukarabati duni na kupuuza sheria za urambazaji.
Zaidi ya watu 300 wameangamia huku takriban 100,000 wakikosa makao.
Mvua inayoendelea kunyesha imesomba mashamba na mazao, na kuzua hofu ya uhaba wa chakula na baa la njaa katika nchi hiyo ambayo tayari inakabiliwa na makali ya janga la Covid-19 na vita nchini Ukraine.