Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji linasema takriban watu 700 waliuawa katika eneo la Darfur Magharibi mwa Sudan kufuatia mapigano kati ya jeshi na vikosi hasimu vya RSF.
Kisa hicho kilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko El Geneina ambapo watu wengine 300 wanaripotiwa kutoweka.
Shirika la haki za binadamu la eneo hilo linakadiria kuwa watu 1,300 waliuawa huko Darfur Magharibi tangu Ijumaa iliyopita na inalaumu RSF kwa ukatili huo.
Haya yanajiri huku RSF ikionekana kuongeza kasi ya mashambulizi katika kanda hiyo.
Mashahidi wanashutumu kundi hilo la wanamgambo na washirika wake kwa kuwalenga watu wasio Waarabu katika maeneo ambayo imeteka.
Shirika la Roots Organization for Human Rights and Violions Monitoring, kundi linalotetea haki za binadamu huko Darfur Magharibi, linaituhumu RSF kwa kuvamia kambi za wwakimbizi na kuanzisha mashambulizi.
RSF hapo awali ilikanusha shutuma hizo.
Kulingana na mashirika ya misaada maelfu ya watu wamekimbilia nchi jirani ya Chad katika siku za hivi karibuni.
Zaidi ya watu milioni tano na nusu wanakadiriwa kufurushwa katika makazi yao tangu ghasia kati ya RSF na Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan kuanza mwezi Aprili.