Polisi nchini Nigeria walisema Jumanne waliwashikilia takriban watu 67 waliokuwa wakisherehekea harusi ya mashoga katika mojawapo ya vizuizi vikubwa zaidi vinavyolenga ushoga, ambao umepigwa marufuku katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
“Washukiwa hao wa jinsia moja” walikamatwa katika mji wa Ekpan kusini mwa jimbo la Delta mwendo wa saa 2 asubuhi siku ya Jumatatu katika hafla ambayo wawili kati yao walikuwa wameoana, msemaji wa polisi wa jimbo hilo Bright Edafe aliwaambia waandishi wa habari. Alisema kuwa ushoga “hautavumiliwa kamwe” nchini Nigeria.
Kukamatwa kwa mashoga ni jambo la kawaida nchini Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambapo mashoga wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 14 jela chini ya Sheria ya Kukataza Ndoa za Jinsia Moja.
Washiriki wanakabiliwa na kifungo cha miaka 10 jela. Sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2013, imelaaniwa ndani na nje ya nchi ingawa inaungwa mkono na watu wengi nchini.
Ofisi ya Amnesty International ya Nigeria ililaani kukamatwa kwa watu hao na kutaka “kukomeshwa mara moja kwa uwindaji huu wa wachawi.”
“Katika jamii ambayo rushwa imekithiri, sheria hii (ya watu wa jinsia moja) inayopiga marufuku mahusiano ya watu wa jinsia moja inazidi kutumika kwa unyanyasaji, unyang’anyi na ulaghai wa watu,” Isa Sanusi, mkurugenzi wa shirika hilo nchini Nigeria, aliiambia Associated Press.
Polisi huko Delta walivamia hoteli moja huko Ekpan ambapo harusi hiyo ya mashoga ilikuwa inafanywa na awali kuwakamata watu 200, Edafe aliwaambia waandishi wa habari na baadaye, 67 kati yao walizuiliwa baada ya uchunguzi wa awali, alisema.