Zaidi ya watu 51 wameuawa katika jimbo la Benue kati kati mwa Nigeria kwa mujibu wa mashahidi na vyombo vya habari vya eneo hilo.
Maiti za wanakijiji waliouawa zimepatikana kutoka kwa jamii ya Umogidi ya Otukpo katika Jimbo hilo baada ya magenge yenye silaha kuwashambulia . Idadi isiyojulikana ya wanakijiji bado inaripotiwa kupotea.
Kiongozi wa vijana wa jamii hiyo Adakole Inalegu Daniel aliambia BBC kuwa wakaazi, ikiwa ni pamoja na vikundi vya vijana bado wanaendelea kuchana vichaka vinavyozunguka eneo hilo kutafuta miili zaidi.
Ripoti zinasema watu wenye silaha walivamia jamii ya wakulima siku ya Jumatano. Walianza kutoka soko la kijiji, wakimpiga risasi mtu yeyote waliyekutana naye. Wakazi wanasema wengi waliokimbilia msituni walimiminiwa risasi na miili yao kukatwa vichwa.
Ingawa vikosi vya usalama vilitumwa katika eneo hilo, uwepo wao haujazuia mashambulizi hayo mabaya.
Wakaazi wa jamii kadhaa za kilimo katika jimbo la Benue wamekuwa katika mapigano makali na wafugaji. Wakulima wanawalaumu wafugaji kwa kutumia mifugo yao kuharibu mazao yao huku wafugaji wakiwashutumu wakulima kwa kushambulia mifugo yao.