Takriban watu 50 wamekufa maji na 167 hawajulikani walipo baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kupinduka kwenye mto Kongo jioni ya siku ya Ijumaa, kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Didier Mbula, waziri wa afya wa mkoa wa Equateur amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, watu 189 wameokolewa na kwamba msako bado unaendelea.
Katika matamshi yake hayo, Waziri Mbule amesema: “Kwa mujibu wa idadi tuliyonayo hadi sasa katika Serikali ya Mkoa, maiti 49 zimeopolewa, 167 hazijapatikana.”
Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika maji ya Kongo hususan kutokana na kuwa vyombo vingi vya majini hupakia watu kupita kiasi. Nchi hiyo ina ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri mkubwa na wa majini. Boti nyingi DRC ni chakavu na zinabeba watu na mizigo kupita kiasi
Naye Naibu Gavana wa jimbo hilo, Taylor Ng'anzi amesema kuwa ajali hiyo imetokea katika mji wa Mbandaka kwenye Mto Kongo katika Mkoa wa Equateur watu wasiopungua 49 wamekufa maji na wengine 120 hawajulikani walipo.
Amesema: "Boti ilikuwa ikisafiri kwenda Bolomba, eneo lililoko umbali wa zaidi ya kilomita 300 kutoka bandari ya Bankita katika mji wa Mbandaka wakati ilipozama usiku." Ameongeza kuwa, safari za usiku za boti ni kinyume cha sheria."
Amesema, "Katika boti hiyo kulikuwa na abiria na mizigo vikiwemo vifaa vya ujenzi, Utafutaji wa watu zaidi unaendelea."
Watu walioshuhudia wamesema kuwa, boti hiyo ya inayomilikiwa na mtu binafsi ilikuwa imebeba mifuko 500 ya saruji na vyuma.
Taarifa zinasema kuwa boti hiyo ilikuwa imetengenezwa kienyeji sana na haikuwa imetimiza viwango vya kubeba abiria. Zaidi ya yote ni kwamba ilikuwa inasafiri usiku, wakati safari za usiku zimepigwa marufuku huko DRC ili kupunguza ajali.