Takriban watu 44, hasa wanamgambo wenye silaha, wameuawa wiki hii wakati yalipozuka mapigano kati ya makundi mawili hasimu huko kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Anadolu ambalo limeandika: "Mapigano kati ya wanamgambo wa AAK Zande na kundi la waasi la Umoja wa Amani la Jamhuri ya Afrika ya Kati (UPC) yalizuka Jumanne asubuhi katika mji wa Mboki wa jimbo la Haut-Mbomou, na kudumaza shughuli za biashara."
Meya Leah Pata ameliambia shirika hilo la habari kwamba idadi ya waliouawa ni watu 44 wakiwemo raia wanne. Amesema, mamia ya raia wamekimbilia maeneo mbalimbali kama ya ibada kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mapigano hayo kati ya vikundi hivyo viwili hasimu yamewalazimisha zaidi ya watu 5,000 kukimbia mjini Mboki na kuelekea katika mji wa Zemio wa jimbo hilo.
Kundi la UPC ni la muungano wa makundi makubwa ya waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Miongoni mwa makundi hayo ni lile la Coalition of Patriots for Change (CPC) linaloongozwa na rais wa zamani, Francois Bozize na ambalo liliundwa mwaka 2020 kabla ya uchaguzi wa rais. Muungano huo umesema katika taarifa kwamba, mapigano yalianza baada ya wanamgambo wa AAK Zande kushambulia maeneo ya UPC.
Lengo la muungano wa UPC ni kuiondoa madarakani serikali ya Rais Faustin Archange Touadera lakini majaribio mbalimbali ya mapinduzi kwa kushirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na baadhi ya mamluki kundi la usalama la Wagner la nchini Russia.
Umoja wa Mataifa umeyalaumu makundi ya waasi kwa kuendeleza vitendo vya ugaidi, kuhatarisha usalama na kuwasababishia mateso raia.