Nigeria imetangaza hali ya dharura kutokana na homa ya Lassa ambayo imepelekea watu 37 wapoteze maisha mwezi Januari huku uchaguzi mkuu ukikaribia nchini humo.
Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Magonjwa (NCDC) kimetoa taarifa na kutangaza kuzinduliwa Kituo cha Kitaifa cha Operesheni za Dharura za Kitaifa cha Homa ya Lassa ili kuratibu na kuimarisha shughuli zinazoendelea za kukabiliana homa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa NCDC Chikwe Ihekweazu amesema hali ya dharura imetangazwa kutokana na tathmini ya hatari iliyofanywa Januari 20 na Kituo hicho.
Amesema mwaka huu kumeshuhudiwa kuongezeka kwa idadi ya kesi zilizothibitishwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Kituo hicho kimesema hadi kufikia Jumatano kulikuwa na jumla ya kesi 244 zilizothibitishwa za homa ya Lassa na vifo 37 vilivyohusiana na homa hiyo.
Taasisi hiyo ya kiafya imetoa mwongozo wa kitaifa wa udhibiti, usimamizi na matibabu ya homa ya Lassa.
Homa ya Lassa ni ugonjwa hatari wa virusi unaoenezwa na panya wa kawaida wa Kiafrika na ni ugonjwa wa kawaida katika mataifa ya Afrika hasa Nigeria, Sierra Leon, Guinea na Liberia.