Zaidi ya watu 24, wakiwemo wanajeshi, waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa siku ya Jumatatu kufuatia shambulio la bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Taarifa zinasema mshambuliaji wa kujitoa mhanga amejiripua katika kituo cha mafunzo ya kijeshi mjini Mogadishu, na kuua zaidi ya watu 20, wakiwemo wanajeshi na makurutu.
Imedokezwa kuwa gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa mabomu alijilipua katika foleni ya makurutu katika kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Jalle Siyaad.
Taaria zinasema makumi ya watu pia walijeruhiwa katika shambulio hilo ambao walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Vyombo vya habari vya ndani viliweka majeruhi kuwa zaidi ya watu 30.
Kundi la kigaidi lenye mafungamano na al-Qaeda lenye makao yake nchini Somalia la Al-Shabaab lilidai kuhusika na shambulio hilo baya.
Hayo yanajiri wakati ambao wanachama wasiopungua 100 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waliuawa hivi karibuni katika operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na vikosi vya kigeni katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wizara ya Habari ya Somalia ilisema magaidi hao wa al-Shabaab waliuawa katika operesheni kabambe iliyofanyika wiki iliyopita Jumatano katika vijiji vya Gal-Libah na El Quraq vilivyopo katika mpaka wa majimbo ya Galgaduud na Middle Shabelle.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, magaidi hao wakiwemo makamanda wao saba wa ngazi za juu wameuawa katika operesheni ya pamoja ya vikosi vya Somalia kwa ushirikiano na askari vamizi wa Marekani.
Kundi la kigaidi la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya kila liwezalo kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007; na hadi kufikia sasa kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi na kuuwa wanajeshi na raia wengi.