Polisi nchini Uganda walisema Jumatatu kuwa watu 20 wamekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na kundi la wanamgambo linalolaumiwa kufanya shambulio wiki iliyopita katika shule iliyoko jirani na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
"Watu 20 wamekamatwa wanauhumiwa kuwa washirika, wanaoshukiwa kushirikiana na ADF," msemaji wa polisi Fred Enanga aliuambia mkutano wa waandishi wa habari, akimaanisha kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) chenye makazi yake nchini DRC.
"Pia tunaye mwalimu mkuu na mkurugenzi wa shule, ikiwa kama sehemu ya uchunguzi wetu . Wanatakiwa watupe majibu ya baadhi ya maswali," aliongeza, bila kuweka wazi kama wamewakamata.
Enanga alisema idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kinyama lililofanyika katika shule ya Sekondari ya Lhubiriha iliyoko Mpondwe katika eneo la mbali huko Magharibi mwa Uganda siku ya Ijumaa ambapo watu 42 waliuwawa, wakiwemo wanafunzi 37.
Watu wengine sita walijeruhiwa na kulazwa hospitali, aliongeza
Rais wa Uganda Joweri Museveni Jumapili aliamuru kupelekwa wanajeshi zaidi katika eneo hilo lililopo magharibi mwa Uganda ambako washambuliaji kutoka kundi lenye uhusiano na Islamic State linatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo ya wanafunzi.
Jeshi na polisi wamesema washambuliaji pia waliwateka wanafunzi sita na kukimbilia kuelekea mbuga ya wanyama pori ya Virunga upande wa pili wa mpaka.
Washambuliaji wamesababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na shirika la maendeleo la serikali za nchi za Afrika. Uganda ilishtushwa na shambulizi hilo.
Baadhi ya taarifa ya habari hii zinatoka katika shirika la habari la AFP