Takriban watu 17 waliuawa na wengine 106 kujeruhiwa Jumatano baada ya roketi kugonga soko kusini mwa mji mkuu Khartoum, muungano wa madaktari wa Sudan ulisema.
Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa kwa kushambuliwa kwa makombora katika mji mkuu tangu mapigano kati ya jeshi la Sudan na Kikosi Maalum cha RSF kuanza tarehe 15 Aprili.
Shambulio hilo limekuja huku mazungumzo yaliyokuwa yakisimamiwa na Marekani na Saudi Arabia kumaliza mzozo huo yakiporomoka.
"Eneo la Mayo [Soko la 6] lilishuhudia mashambulizi makali na ya umwagaji damu mchana huu, ambayo yalisababisha vifo vya watu 17 na zaidi ya 106 kujeruhiwa," Shirika la Madaktari wa Sudan lilisema katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Inafikisha idadi ya vifo vya raia katika vita hivyo kufikia 883.