Watoto wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wengine wawili kujeruhiwa katika harakati ya kulipiza kisasi mjini Isiolo.
Watoto hao walipigwa risasi kuuawa na watu wenye silaha Jumamosi iliyopita jioni katika Kijiji cha Ngarendare kilichopo Kaunti ya Isiolo katika harakati zinazodhaniwa kuwa ni kulipiza kisasi.
Watoto hao, Lipe Lemantile (5) na Naiku Lemantile (6) walishambuliwa katika kijiji chao cha Ngarendare baada ya watu wasiojulikana waliokuwa na silaha kuvamia kijiji chao huko Oldonyiro.
Watu hao wenye silaha pia waliwapiga risasi na kuwajeruhi wanakijiji wengine wawili ambao wamelazwa katika Hospitali ya Kaunti ya Isiolo wakiwa katika hali mbaya.
Watu hao ambao polisi wanashuku walifanya tukio hilo kama namna ya kulipiza kisasi, walitoroka bila kuiba wala kupora chochote kijijini hapo.
Vyombo vya usalama vilihamasishwa kuwafuata washambuliaji hao bila mafanikio.
Maofisa wanahofia kutakuwa na ulipizaji kisasi zaidi kutoka eneo lililoathiriwa huku kukiwa na mwito wa kuchukuliwa hatua ili kudhibiti hali hiyo.
Huko Maikona, Kaunti ya Marsabit, mzee wa miaka 60 alipigwa risasi na kujeruhiwa katika shambulio la watu wenye silaha.
Kwa mujibu wa polisi, wapiganaji hao walikuwa wakilenga mifugo katika kijiji hicho, lakini walirudishwa nyuma na askari wa akiba wenye silaha wa eneo hilo.
Polisi walisema Bakala Ramata mwenye umri wa takribani miaka 60, alipata jeraha la risasi kichwani na alipelekwa katika Hospitali ya Kalacha.
Mkuu wa polisi wa eneo la Mashariki, Rono Bunei alisema mapigano hayo yanazidi kuwa mabaya kwani yanatishia uthabiti wa eneo hilo.
“Tunawaomba viongozi wa eneo hilo kuja pamoja na kushughulikia tishio hili,” alisema na kuongeza kuwa, walikuwa wametuma timu kuwafuata washambuliaji.
Mapigano hayo na kuibiwa kwa wanyama ni sehemu ya chuki inayoendelea kati ya jamii katika eneo hilo ambayo imesababisha vifo vya watu wengi na wengine kuyahama makazi yao mwaka uliopita.
Sehemu nyingi za Marsabit zilikuwa chini ya amri ya kutotoka nje hadi siku ya uchaguzi wakati zoezi hilo lilipokamilika.