Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wanne waliokwama kwenye jokofu nchini Namibia wafariki

Watoto Wanne Waliokwama Kwenye Jokofu Nchini Namibia Wafariki.png Watoto wanne waliokwama kwenye jokofu nchini Namibia wafariki

Wed, 18 Sep 2024 Chanzo: Bbc

Polisi nchini Namibia wanachunguza kifo cha watoto wanne waliokuwa wakicheza kwenye jokofu tupu katika mkoa wa Zambezi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Watoto hao waliokuwa na umri wa kati ya miaka mitatu na sita, walipatikana ndani ya jokofu lililotumika katika eneo lenye watu wengi katika mji wa Katima Mulilo siku ya Jumatatu alasiri.

Polisi wanaamini kuwa watoto hao walikwama kwenye jokofu kwa bahati mbaya walipokuwa wakicheza lakini uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo.

Kati ya watoto hao wanne, wawili walikosa hewa hadi kufa kwenye jokofu huku wengine wawili wakifia hospitalini wakipokea matibabu, shirika la utangazaji la umma liliripoti.

"Nilipoingia, niliwaona wahudumu wa afya wakihudumia binti yangu na msichana mwingine. Waliwakimbiza hospitalini, huku wengine wawili wakiwa wamepakiwa kwenye magari ya polisi ya kuhifadhia maiti,” Aranges Shoro, mmoja wa baba wa watoto hao, aliliambia gazeti la kibinafsi la The Namibian.

"Kulikuwa na ndoano kwenye jokofu ambayo inaweza kufunguliwa kutoka nje tu," kamanda wa polisi wa eneo la Zambezi Andreas Shilelo alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema.

"Walikwama kwa muda wa saa moja na nusu na kukosa hewa."

Chanzo: Bbc