Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto nusu milioni Malawi hatarini kukumbwa na utapiamlo

Pic Utapiamlo Data.jpeg Watoto nusu milioni Malawi hatarini kukumbwa na utapiamlo

Sat, 20 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takribani watoto 573,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Malawi wako hatarini kukumbwa na utapiamlo, limetangaza shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF huku likisema linahitaji dola milioni 87.7 kukidhi mahitaji ya watu milioni 6.5 wakiwemo watoto milioni 3.3 nchini humo.

UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa jijiini Lilongwe jana Ijumaa, imasema maendeleo yaliyopatikana hivi karibuni ya kukabili utapiamlo yanayoyoma kutokana na uhaba mkubwa wa chakula unaoandamana na matukio ya mara kwa mara ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa yanayozuilika, ukosefu wa utulivu wa kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ufadhili kwenye sekta za kijamii.

Taarifa hiyo inasema Malawi bado inazingirwa na kiza kinene cha athari mbaya za kimbunga Fredy kilicholikumba taifa hilo mwezi Machi na kuacha watu 659,000 wakiwa wakimbizi wa ndani, wakiwemo watoto.

Halikadhalika mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu bado unaendelea na tayari umesababisha vifo vya watu 1,759.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Malawi, Gianfranco Rotigliano, anasema watoto nchini humo wanakabiliwa na mlolongo wa majanga. Ukosefu wa uhakika wa kupata chakula ukichochewa na janga la mabadiliko ya tabianchi, mlipuko wa magonjwa na mdororo wa uchumi duniani, vyote vinatishia maisha ya mamilioni ya watoto.

Amekariri ombi la Hatua za Kiutu kwa Watoto, HAC lililozinduliwa leo na UNICEF likionesha ongezeko la matukio ya utapiamlo miongoni mwa watoto katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo mwaka 2023 pekee watoto 62,000 wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi miaka 5 wako hatarini kukumbwa na unyafuzi au udumavu.

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF imeongeza ombi lake kwa usaidizi Malawi kutoka zaidi ya dola milioni 52 hadi dola milioni 87 ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 6.5 wakiwemo watoto milioni 3.3.

Fedha hizo zitatumika kununua mahitaji ya vyakula vilivyo tayari kuliwa ili kutibu unyafuzi, kupata huduma za maji safi na salama, huduma za kujisafi, afya, lishe, elimu, ulinzi dhidi ya watoto na miradi ya fedha taslimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live