Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto milioni 1 Mali hatarini kukabiliwa na utapiamlo

Njaaaa Watoto milioni 1 Mali hatarini kukabiliwa na utapiamlo

Sun, 3 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takribani Watoto milioni moja wenye umri wa chini ya miaka 5 nchini Mali wako hatarini kutumbukia kwenye utapiamlo uliokithiri kutokana na mchanganyiko wa mizozo ya muda mrefu, ukimbizi wa ndani na vikwazo vya kufikisha misaada ya kibinadamu.

Taarifa ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inasema kati ya watoto hao milioni moja, watoto 200,000 wako hatarini kufa kwa njaa iwapo misaada ya kuokoa maisha haitawafikia.

“Takribani robo ya watoto wote nchini Mali wanakabiliwa na ukosefu mkubwa au wa kati wa chakula. Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza nchini humo, zaidi ya watu 2,500 wako hatarini kukumbwa na baa la njaa kwenye eneo la Menaka linalokabiliwa na mzozo, na nusu yao ni watoto,” imesema taarifa hiyo ya Mfuko wa Dharura wa Watoto wa Umoja wa Mataifa, UNICEF.

Onyo hilo la UNICEF linakuja wakati maafisa waandamizi wa UNICEF na wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP wametembelea nchi hiyo siku chache zilizopita kusisitiza usaidizi wa mashirika hayo kwa wananchi wa Mali kwa ushirikiano na serikali na wadau wa kibinadamu.

Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF anayehusika na hatua za kibinadamu na operesheni za usambazaji wa misaada amesema, "Mali inapitia kipindi kigumu cha janga la kibinadamu na inahitaji msaada ili kuepusha janga kwa watoto ambao kwa mara nyingine tena wanalipa gharama kubwa ya janga ambalo hawajalisababisha."

Ameongeza kuwa UNICEF, WFP na wadau wengine wamekuwepo nchini Mali wakati wa kipindi kigumu cha mapito nchini humo na wataendelea kufanya kazi kushughulikia masuala ya kibinadamu na maendeleo alimradi huduma hizo zinahitajika.

Kwa ujumla, takribani watoto milioni 5 nchini Mali wanahitaji kwa dharura misaada ya kibinadamu, mathalani afya, lishe, elimu na huduma za ulinzi.

Idadi hiyo ni ongezeko la angalau watoto milioni 1.5 tangu mwaka 2020. Pamoja na mapigano na ghasia, madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika baadhi ya maeneo ya Mali, yamechochea watu kukimbia makazi yao katika miezi ya hivi karibuni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live