Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wategemea mapinduzi kibiashiara kuja ndege ya mizigo

11191bcc8e332a3730c8c5b6dfd41d51 Wategemea mapinduzi kibiashiara kuja ndege ya mizigo

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA na wadau wanaosafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi wamezungumzia ahadi ya serikali ya kununua ndege ya mizigo wakisema italeta mapinduzi makubwa katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

Wakizugumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau hao walisema hatua hiyo itaepusha usumbufu na kuokoa mapato ambayo yamekuwa yakipotea kutokana na kupitisha bidhaa katika nchi jirani kwenda ughaibuni.

Akizindua Bunge la 12 hivi karibuni, Rais John Magufuli alisema serikali itafanya upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na kununua ndege mpya tano ikiwamo ndege moja ya mizigo.

Katibu wa Umoja wa Wavuvi Tanzania (Tanzania Fishers Union-TAFU), Jephta Machandalo, alisema mchakato mrefu wa usafirishaji wa mazao ya samaki nje ya nchi umekuwa ukisababishia wavuvi hasara kutokana na wasafirishaji kununua mazao ya samaki kwa bei ya chini kufidia gharama za usafirishaji.

Alisema wamekuwa wakisafirisha kwa malori kutoka Mwanza kwenda Kenya au Uganda kupata usafiri wa ndege kwenda masoko mbali mbali duniani.

Meneja Mazingira na Biashara wa Umoja wa Wakulima wa Mboga na Maua Tanzania (TAHA),Kelvin Remen alisema ndege ya mizigo ni ukombozi kwa wakulima, itawezesha kuuza bidhaa zao kwa wakati katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Mkurugenzi mtendaji wa TAHA, Jackline Mkindi alisema

katika kipindi chote ambacho Tanzania imekuwa ikisafirisha mizigo kwa kutumia ndege za nje ambazo ni za abiria hivyo sehemu inayopatikana kwa ajili ya mizigo ni ndogo.

“Tukiwa na ndege yetu tunaamini itatusaidia kuwa na safari za uhakika kwenda katika soko letu la Ulaya…Mpaka sasa tunategemea njia moja tu ya Kilimanjaro hadi Liege nchini Ubelgiji baada ya njia ya Kilimanjaro hadi Amsterdam nchini Uholanzi kufungwa kwa sababu ya corona,” alisema Mkindi.

Alisisitiza, “Tukiwa na ndege yetu tunaweza kuzungumza na kupata ruti nyingine kupanua soko.” Alisema katika Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), mizigo inayotoka kwa wiki ni tani 50 na kwa mwezi ni tani 200.

Akizungumzia hali ya usafirishaji mizigo katika Kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere, Meneja Mizigo wa Swissport, Wandwi Mugesi alisema mizigo inayotoka na kuingia kwa wiki ni tani 250 hadi 300.

Alisema mizigo inayotoka pekee ni tani 100 kwa wiki ambazo ni mjumuisho wa bidhaa mbalimbali kama vile maua, samaki na mbogamboga.

Wandwi alitaja changamoto zinazokabili sekta ya mizigo kuwa ni pamoja na ukosefu wa ndege ya ukakika ya mizigo inayoenda moja kwa moja katika masoko ya Ulaya hali inayosababisha kutegemea ndege za abiria.

Pia ukosefu wa nafasi ya kutosha ya mizigo kwa kuwa ndege za mizigo zinatengewa nafasi ya tani 20 ya mizigo ikijumuisha mizigo ya abiria. Hii inasababisha baadhi ya siku kukosa nafasi ya mizigo kwa kuwa mizigo ya abiria inakuwa imechukua nafasi yote.

“Gharama kubwa za usafirishaji ni moja ya changamoto kwa sababu mizigo mingine inalazimika kupandishwa malori kwa sababu ndege hizo hazifiki mikoani kama vile samaki kutoka mwanza kwenda Ulaya,” alisema Wandwi.

Alisema ndege zinazotumika kusafirishia mizigo ni Emirate, Qatar Airways, Turkish Airline, Ethiopian Airways na Kenya Airways. Alisisitiza kuwa wafanyabiashara wanatamani kuwapo ndege inayokwenda moja kwa moja Ulaya katika soko badala ya inayotua njiani kwani mizigo huchelewa.

Alishauri serikali kuwa pindi ndege hiyo ikinunuliwa ijipange kupitia kwa mabalozi wake wote duniani kuteka soko lote la mizigo nje ya nchi ndege ipate mizigo ya kutosha kuepuka kujiendesha kwa hasara.

Mwenyekiti wa Jumuia ya Wavuvi ( Fishers Unions Organization-FUO) mkoani Mwanza, Juvenary Matagili, alishauri ndege itakaponunuliwa, serikali itoe fursa kwa kila mfanyabiashara mwenye uwezo kusafirisha bidhaa zake.

Mwenyekiti wa Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Wilaya ya Kibiti/Rufiji mkoa wa Pwani, Maximillian Masero, alisema uamuzi wa kununua ndege ya mizigo ni malengo mapana ya serikali yatakayoendeleza mapinduzi makubwa kiuchumi.

Desemba mwaka jana, Rais John Magufuli alipopokea ndege mpya ya nane aina ya Bombardier Dash 8 Q400, mjini Mwanza, ndipo kwa mara ya kwanza alieleza mpango wa serikali wa kununua ndege ya mizigo isafirishe maua, minofu ya samaki na nyama kwenda nje.

Katika juhudi za kuwezesha usafirishaji mizigo nje, Mei mwaka huu, serikali ilizindua usafirishaji wa mizigo kwenda Ulaya. Tani nane za minofu ya samaki zilisafirishwa kwenda Brusels nchini Ubelgiji kwa kutumia ndege ya Rwanda.

Chanzo: habarileo.co.tz