Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watazamaji: Uchaguzi Uganda ulikuwa huru, haki

Ed9220a7caacf56dd532161b7f398bfb Watazamaji: Uchaguzi Uganda ulikuwa huru, haki

Tue, 19 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAZAMAJI wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU), wamepongeza mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu nchini Uganda na kusema ulikuwa huru na wa haki.

Mkuu wa Ujumbe wa EAC, Domitien Ndayizeye, alisema kwa jumla uchaguzi ulikuwa huru na haki japo kulikuwapo dosari ndogondogo.

Alisema wametoa mwito kwa mamlaka za nchi hizo kuzifanyiakazi changamoto hizo ili kuboresha zaidi uchaguzi mwingine ujao kwani hakuna uchaguzi unaofanyika kwa asilimia 100 bila changamoto.

Alisema moja ya changamoto ilikuwa ni kuzimwa mitandao ya kijamii jambo ambalo halikuwa la lazima na kwamba, wameitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha inaandikisha wapiga kura wote wanaotimiza umri wa miaka 18 kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Ujumbe huo pia umeisisitiza tume hiyo kuzingatia wakati unaofaa wa utoaji wa hati za kuruhusu watazamaji wa ndani ili kuwezesha uangalizi makini katika chaguzi zijazo.

Akizungumza jijini Kampala juzi wakati akiwasilisha taarifa ya awali ya Ujumbe wa Watazamaji wa Uchaguzi wa EAC kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini Uganda uliofanyika Uganda Januari 14, Ndayizeye ambaye ni Rais wa zamani wa Burundi aliitaka tume ya uchaguzi kuweka mikakati mizuri ya kusimamia mchakato wa upigaji kura iwapo kutatokea hali mbaya ya hewa katika siku ya uchaguzi.

Alisema tume hiyo inapaswa kuweka miongozo ya wazi juu ya uwajibikaji wa vifaa vyote vya kupigia kura na hasa karatasi za kura.

Kuhusu kuzimwa kwa mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi, ujumbe huo ulisema hatua hiyo inakiuka uhuru na haki ya kupata habari kama ilivyoainishwa katika Katiba.

Alisema kuzimwa kwa mitandao pia kuliwaathiri kwani timu zake za watazamaji zilishindwa kupeleka matokeo yao kwa wakati katika kituo kikuu Kampala.

Aidha, ujumbe huo wa EAC umelishauri Bunge la Uganda kurekebisha sheria ya ufadhili wa kampeni kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu matumizi ya fedha za kampeni ili kuweka uwazi katika mchakato wa uchaguzi.

Ndayizeye aliitaka serikali ya Uganda kupitia upya hatua zilizochukuliwa dhidi ya vyama vya upinzani na wagombea wake hususan katika vyumba vya habari hasa radio na televisheni ili kuwa na uchunguzi wa kisiasa.

"Serikali inapaswa pia kukagua utendaji wa huduma za usalama katika mchakato wa uchaguzi na kubainisha changamoto zake zilizosababisha matumizi mabaya ya nguvu na upendeleo dhidi ya vyama vya upinzani na wagombea wake," alisema.

Ujumbe huo pia ulivitaka vyama vyote vya kisiasa kuendelea kukuza ushindani wa kisiasa kwa njia ya amani.

Ujumbe huo ulisema licha ya dosari hizo, siku ya kupiga kura wananchi walionesha kiwango kikubwa cha ukomavu wa demokrasia.

"Upigaji kura ulikuwa wa amani sana na hakuna vitisho vya wapiga kura vilivyotokea. Kanuni za upigaji kura zilizingatiwa kwa kiasi kikubwa,” ulisema ujumbe huo katika ripoti hiyo ya awali.

Wakati wa uchaguzi huo, Waangalizi wa Uchaguzi wa EAC walisambaa katika maeneo mbalimbali kuanzia Januari 12 hadi Januari 15 waliporudi makao makuu ya ujumbe huo Kampala na kuandaa ripoti yao.

Watazamaji wa AU

Kwa upande wake, Ujumbe wa Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) katika uchaguzi huo uliokuwa ukiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Cameroon, Dk Samuel Azu’u Fonkam, ulisema uchaguzi ulifanyika kwa amani na walishuhudia idadi kubwa ya vijana na wanawake katika vituo vya kupigia kura.

Ujumbe huo umewahimiza wadau wote wa uchaguzi hasa viongozi wa kisiasa kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha kupoteza maisha na uharibifu wa mali.

"Ujumbe unatambua kwamba uchaguzi unakuja na kuondoka lakini ,Uganda na raia wake wanabaki. Unahimiza wadau kushiriki mazungumzo ya amani katika ngazi zote na kuondoa migogoro yote kwa amani kulingana na taratibu zilizowekwa,” alisema Dk Fonkam.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa chama cha NRM, Yoweri Museveni alichaguliwa kuwa Rais wa Uganda kwa kipindi cha sita baada ya kupata asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa.

Museveni ametangazwa Rais baada ya kupata kura 5,851,037 ya kura zote zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake mkuu, mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.

Chanzo: habarileo.co.tz