TANZANIA na Burundi ni nchi majirani ambazo zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya faida ya nchi hizo na wananchi wake.
Katika kuhakikisha hilo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Maleko ametaja bidhaa mbalimbali zinazohitajika nchini Burundi na nyingine kusafirishwa mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ametaja baadhi ya bidhaa zinazohitajika ni mchele, mtama mweupe, mahindi, unga wa mahindi, muhogo uliokaushwa (makopa) na unga wa muhogo (udaga), maharage, mafuta ya kupikia, chumvi yenye madini joto, mvinyo na vifaa vya ujenzi kama saruji, vigae, mabati na nondo, ambavyo vyote vinapatikana kwa wingi nchini.
Amesema bidhaa nyingine zinazohitajika nchini humo ni magodoro, vilainishi vya mitambo na malighafi za kutengenezea mbolea na saruji na kwamba pia husafirishwa kwenda Jimbo la Kivu Kusini lililopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inayopakana na nchi hiyo.
Ameekeza kuwa, thamani ya bidhaa za Burundi zilizouzwa Tanzania mwaka 2019 ilifikia Sh milioni 831.4, huku Tanzania ikiuza bidhaa nchini humo zenye thamani ya Sh bilioni 200.18.
Amesema kwa sasa hali ya kisiasa na kiusalama nchini humo ni tulivu na hali ya uchumi inaanza kutengamaa na kuwa fursa nzuri ya kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii ya nchi zote mbili.
Kutokana na maelezo hayo ya Balozi Dk Maleko, ni dhahiri kuwa bidhaa nyingi zilizotajwa kuhitajika nchini humo zinapatikana Tanzania kwa wingi, hivyo ni fursa kwa Watanzania kukamata fursa hiyo ya kuepeleka bidhaa nchini humo.
Kama alivyosema Balozi huyo, hali ya usalama nchini humo kwa ujumla ni shwari, kwani kwa muda mrefu wafanyabiashara wengi wamekuwa na hofu ya kufanya biashara kwa kuhofia vita na mapigano.
Ni wakati sasa kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizo kabla ya watu kutoka nchi nyingine kuja nchini kuchukua bidhaa na kuuza kwenye maeneo hayo huku Watanzania wakibaki kuuza ndani kwa gharama nafuu.
Katika kuhakikisha fursa hiyo inafanyiwa kazi ni vama mamlaka zinazohusika kusaidia Watanzania katika kufanya biashara halali kwa manufaa ya nchi kwani uhitaji unavyoongezeka ndivyo baadhi ya watu wasio waaminifu wanaweza kutumia fursa hiyo vibaya.
Katika kuhakikisha fursa hiyo inatumika vizuri, ni vema pia makundi ya wafanyabiashara wanawake, vijana na wengineo kufanya biashara na nchi jirani ikiwa ni katika kuimarisha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wananchi wa nchi za EAC kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakisisitizwa kufanya biashara ndani ya ukanda huu hivyo ni dhahiri kuwa Burundi itapokea bidhaa kutoka Tanzania kuliko zinazotoka nchi nyingine za mbali kwani hata gharama kwa zitakuwa ndogo kutokana na ukaribu wa nchi hizo.
Pia, bidhaa hizo kuingizwa kutoka Tanzania zitaendelea kukuza uhusiano wa kidiplomasia na uchumi baina ya nchi hizo mbili jirani zenye uhusiano wa kindugu kutokana na mengi ambayo Tanzania imefanya wakati Burundi ikiwa kwenye migogoro.