Raia watano waliuawa siku ya Jumanne jioni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika shambulio lililohusishwa na waasi wa ADF, wanaoshirikiana na kundi la Islamic State, kulingana na shirika la habari la AFP, likinukuu vyanzo vya ndani siku ya Jumatano.
Waasi walifanya uvamizi mwendo wa saa 2:00 katika eneo la Ngite, katika wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Jadot Mwendapole, afisa wa mashirika ya kiraia katika eneo hilo, ameliambia shirika la habari la AFP.
"Waliwaua raia watano, wote wanaume, wengine kwa silaha za moto, wengine kwa visu," ameongeza, akifafanua kuwa mtu mwingine hajulikani aliko na kwamba washambuliaji walipora mali kadhaa. "ADF waliua raia watano," amesema Augustin Kapupa, mkuu wa eneo la Mbau, ambako Ngite inapatikana.
Kundi la waasi la ADF (Allied Democratic Forces), lenye Waislamu wengi kutoka Uganda, limeanzishwa tangu katikati ya miaka ya 1990 mashariki mwa DRC, ambapo wameua maelfu ya raia. Walitangaza kujiunga na IS mwaka 2019, IS inalichukulia kama tawi lake "ukanda wa Afrika ya Kati".
Mwishoni mwa 2021, baada ya mashambulizi yaliyohusishwa na ADF katika ardhi ya Uganda, Kampala na Kinshasa zilianzisha operesheni ya pamoja ya kijeshi dhidi yao, iliyoitwa "Shujaa", lakini ADF inaendelea na ukatili wao.
Mnamo mwezi Desemba 2023, walituhumiwa kufanya mashambulizi mawili magharibi mwa Uganda, ambapo wanakijiji 13 waliuawa.