Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watalii waanza kusepa Kenya, Odinga adai kutishiwa kuuawa

Odinga Maandamano G.jpeg Watalii waanza kusepa Kenya, Odinga adai kutishiwa kuuawa

Thu, 23 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbali na hasara ya Sh. bilioni mbili inayotajwa kupotea kutokana na maandamano yaliyofanyika nchini Kenya mwanzoni mwa wiki hii, inaelezwa kuwa sekta ya utalii imeathirika zaidi kutokana na watalii wengi kuanza kuondoka wakihofia usalama wao.

Jana katika mitandao ya kijamii kilirushwa kipande cha video kinachoonyesha msururu wa raia wa kigeni wakiwa wamebeba mabegi wakiingia katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, wakifanya jitihada za kutaka kuondoka nchini Kenya wakihofia machafuko yaliyosababishwa na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati wa maandamano.

Imeelezwa kuwa hali hiyo itasababisha hasara kubwa katika hoteli za kitalii, sekta ya utalii na taifa la Kenya kwa ujumla, na pamoja na matokeo hayo, kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametoa wito kwa wafuasi wake kufanya maandamano mara mbili kwa wiki hadi serikali itakapofanyia kazi madai yao.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Jumatatu wiki hii Odinga aliitisha maandamano yanayotajwa kusababisha ghasia katika maeneo mbalimbali nchini humo hasa jiji kuu la Nairobi na Kisumu, huku polisi wakisema mwanafunzi mmoja aliuawa na wengine 200 kukamatwa.

Sababu ya Odinga kuitisha maandamano hayo ni kuipinga Serikali ya Rais William Ruto kuhusu kupanda kwa gharama za maisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, Japheth Koome, baadhi ya waandamanaji waliwasha moto mitaani na kuwarushia mawe polisi.

Alisema Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kuwarushia maji yanayowasha waandamanaji hao ukiwamo msafara wa Odinga aliyekuwa akiwahutubia wafuasi wake kutoka kwenye paa la gari yake.

Pia, alisema maofisa 24 walijeruhiwa katika mapambano hayo, lakini hawakutoa idadi ya waandamanaji waliojeruhiwa.

“Mapambano hayo ya siku nzima yaliyoshuhudiwa huko Nairobi na Kisumu hayakuwa na msingi zaidi ya kufanya ghasia dhidi ya polisi na kuhujumu uchumi,” alisema.

MADAI YA KUUAWA

Hata hivyo, Kiongozi wa Azimio Odinga, alidai kuwa kulikuwa na jaribio la maofisa wa usalama kumwangamiza yeye pamoja na Kalonzo Musyoka wakati wa maandamano ya Jumatatu.

Alisema maofisa wa usalama waliwafyatulia magari yao risasi wakati wa maandamano jijini Nairobi jambo ambalo liliwashtua.

“Kulikuwa na jaribio la kuangamiza Raila Odinga na Kalonzo Musyoka. Magari yao yalilengwa na risasi, lakini kwa bahati mzuri hawakupata majeraha. Tunaendelea kushangazwa na kitendo hicho cha polisi,” alisema Odinga.

ODINGA AKAMATWE

Kutokana na ghasia hizo, wabunge wa chama tawala UDA waliitaka serikali kumchukulia hatua na kumkamata kinara wa Azimio Odinga kwa madai kuwa maandamano aliyoyaitisha yalisababisha uharibifu wa mali za Wakenya.

Wabunge hao walitoa taarifa kwa wanahabari wakiongozwa na Gavana Cecil Mbarire, wakisema kuwa Odinga, aliongoza maandamano yaliyoleta vurugu sehemu kadhaa katika taifa hilo.

“Jumatatu Raila aliongoza kundi lake la waporaji kutatiza amani na utulivu wa Jiji la Nairobi na sehemu kadhaa nchini. Odinga aliongoza vurugu iliyosababisha kuharibiwa kwa mali na kutatizika kwa biashara nchini,” alisema Mbarire.

Wabunge hao wa UDA pia walitoa wito kwa vitengo vya usalama kuanzisha mchakato wa kumshtaki Odinga na viongozi wengine wa mrengo wa Azimio kwa uharibifu wa mali na maisha yoyote yaliyopotezwa wakati wa maandamano.

“Wao kama Azimio wanastahili kushtakiwa kwa uharibifu na uporaji wa mali na pia kwa maafa yoyote yaliyompata mtu wakati wa maandamano,” alisema Mbarire.

Vile vile, Mbarire aliwapongeza maofisa wa usalama ambao anasema walifanya kazi nzuri iliyohakikisha kuwa utulivu unarejea licha ya purukushani iliyoshuhudiwa.

VIONGOZI WA DINI

Baadhi ya viongozi wa Kiislamu wametoa wito kwa Odinga kusitisha maandamano wakati wa ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani

Katibu wa Muungano wa Maimamu nchini humo, Shekhe Mohamed Khalifa, alisema wanatarajia kuanza kufunga kwa maombi ya mwezi wa Ramadhani kuanzia leo, Machi 23.

Katibu huyo alimtaka Raila kuwaheshimu waislamu watakaokuwa wanafunga kwa maombi kwa kusitisha maandamano aliyoyaitisha.

“Wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Mwenyezi Mungu huweka kando mashetani yote ili kumpa muislamu wakati mwafaka wa kuswali, waheshimu waislamu kwamba ni mwezi wao wa ibada, tunawasihi wale wote wanaohusika katika mipango hii ya maandamano kuuheshimu mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na pia kuwaheshimu waislamu,” alisisitiza Khalifa.

Shekhe Mohammed Dor, miongoni mwa viongozi wa kiislamu, alisema kuwa ipo haja ya makubaliana na maelewano ya haraka kuhusu mzozo unaoshuhudiwa.

“Kuna haja ya kutafuta mbinu mwafaka itakayoweza kusuluhisha mzozo unaoendelea na kuwapa fursa Wakenya muda mwafaka wa kubuni njia za kujenga uchumi wa taifa,” alisema Dor.

Aidha, viongozi wengine wa madhehebu mbalimbali wamejitokeza na kuomba kuwe na makubaliano kati ya makundi mawili ya kisiasa yanayozozana kwa manufaa ya maendeleo ya taifa hilo.

Katibu Mkuu wa chama tawala (UDA), Cleophas Malala, alidokeza kuwa kuna uwezekano wa maridhiano kati ya Rais Ruto na mpinzani wake Odinga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: