- Watahiniwa hao wa shule ya wavulana ya Anestar waliwavamia wenzao wa kike wa shule ya Anesta Precious Girls
- Wasichana hao walipiga kamsa na maafisa kutoka kituo cha Polisi cha Githioro wakafika kwa haraka kuwaokoa
- Watahiniwa hao kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha Dundori wakisubiri uchunguzi kukamilika
Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani baada ya wanafunzi wa kiume katika shule ya Anestar Boys Kaunti ya Nakuru kuwavamia wenzao wa kike majira ya usiku.
Tukio hilo lilisababisha kukamatwa kwa wanafunzi 10 ambao ni watahiniwa wa KCSE kutoka Anestar Bahati Boys waliovunja na kuingia katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Anestar Precious Girls.
Wanafunzi hao walitoroka shuleni mwao na kupenyeza hadi katika shule ya wasichana hao.
Kulingana na Idara ya Upelelezi (DCI), wasichana hao walipiga kamsa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Polisi cha Githioro wakafika kwa haraka.
Hata hivyo kuwasili kwa maafisa wa polisi shuleni humo hakukuwazuia wavulana hao kuzurura mabwenini mwa wasichana hao.
Watahiniwa hao kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha Dundori wakisubiri uchunguzi kukamilika.
Matukio kadhaa yameripotiwa wakati wa kipindi cha mitihani ya kitaifa mwaka huu.
Siku ya Alhamisi, Aprili 9, kulishuhudiwa hali ya mshikemshike baada ya mtahiniwa aliyekuwa akiufanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha Nne (KCSE) kuwakabili maafisa wa polisi waliomtaka kuvalia maski.
Mwanafunzi huyo kutoka Shule ya Sekondari ya mseto ya Karigu-Ini aliripotiwa kukataa kuvaa maski na wakati afisa wa polisi alipoingilia kati, alizua fujo.
Kulingana na ripoti ya polisi TUKO.co.ke, mwanafunzi huyo alimkabili afisa huyo huku akimtupia matusi makali.
Wakati afisa mwingine wa usalama aliingia kati, mwanafunzi alihepa darasani humo, akachukua jiwe na kugonga kioo cha mbele cha gari la polisi.
Alitoweka vichakani na kukosa kuufanya mtihani wa CRE.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.