Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu UN waitia hatiani Rwanda kuwafadhili M23

DRC CRWANDA WAKUTANA TENA Wataalamu UN waitia hatiani Rwanda kuwafadhili M23

Fri, 5 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vikosi vya jeshi la Rwanda viliwashambulia askari ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na vililisaidia na kulipatia na silaha kundi la waasi wa M23.

Hayo yameelezwa na ripoti ya jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa ambao wamesisitiza kwamba kuna "ushahidi madhubuti" wa kuthibitisha madai hayo licha ya ukanushaji wa mara kwa mara unaofanywa na serikali ya Kigali.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikiishutuma Rwanda kila mara kuwa inawasaidia wanamgambo wa M23, ambao katika miezi ya karibuni wameyateka maeneo kadhaa ya ardhi ya Kongo. Hata hivyo Rwanda imekuwa ikikanusha kuliunga mkono kundi hilo; na M23 yenyewe imekuwa ikisisitiza kuwa haiungwi mkono wala kupatiwa misaada yoyote na serikali ya Kigali.

Hata hivyo ripoti ya kurasa 131 iliyotolewa na wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa Kigali "imetoa msaada kwa vikosi vya M23 kwa operesheni maalum", hasa "kuteka miji na maeneo ya kimkakati" huko DRC

Ripoti hiyo imeashiria kama mfano, kutekwa kwa mji wa Bunagana na waasi tarehe 13 Juni mwaka huu, mkoani Kivu Kaskazini. Katika vielelezo vyao, wataalamu hao wamekusanya picha za ndege zisizo na rubani, video na picha na ushahidi wa mashuhuda. Ushahidi huo unafichua safu kubwa za wanajeshi mia kadhaa karibu na mipaka ya DRC, Rwanda, Uganda, wakitembea huku wamevalia sare zinazofanana na za wanajeshi wa Rwanda.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo imeendelea kufichua kuwa, wiki mbili kabla ya shambulio la Bunagana, kambi ya jeshi la DRC ya Rumangabo ilishambuliwa kwa makombora na risasi na kuongeza kuwa: "wanamgambo wa M23 na wanajeshi wa Rwanda walishambulia kwa pamoja". Aidha, ripoti hiyo imesema safu za wanajeshi 900 hadi 1,000 wa Rwanda "zilikata barabara kuu ya RN12 na kushambulia, kisha kuwaondoa wanajeshi wa FARDC kwenye ngome zao".

Msemaji wa serikali ya DRC Patrick Muyaya amekaribisha kazi iliyofanywa na wataalamu hao wa UN akisema: ukweli hatimaye hushinda. Muyaya ameeleza katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter kwamba: wana matumaini ya kufikiwa haraka hitimisho la kukomesha uingiliaji wa Rwanda na kurejesha amani ya kudumu.

Kwa upande wa msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, yeye ameeleza katika taarifa kwamba, serikali ya Kigali haitatoa maoni yoyote kwa kile alichokiita "ripoti isiyo na itibari na ambayo haijatolewa rasmi hadharani"

Chanzo: www.tanzaniaweb.live