Maafisa waandamizi kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameanza kukutana jijini Luanda, Angola kabla ya Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo ambapo Tanzania pia inashiriki.
Ufunguzi wa mkutano huo umefanyika Agosti 8, 2023 ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekabidhi uenyekiti wa ngazi hiyo kwa Angola ambayo itashikilia wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Agosti 2024.
Tanzania ambayo ni moja ya nchi waasisi wa SADC inashiriki kikamilifu Mkutano huo na kwa ngazi ya maafisa waandamizi, ujumbe wake unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Shaban.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Balozi Songhu Kayumba amesema kwa mwaka mmoja wa uenyekiti wa DRC, nchi wanachama ziliunganisha nguvu kuhakikiasha kuwa wanafikia malengo waliyojiwekea kupitia kaulimbiu Kuhamasisha Uwekezaji katika viwanda kupitia usindikaji wa mazao ya kilimo, madini, kuendeleza mnyororo wa thamani wa kikanda kwa nia ya kufikia uakuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.”