Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, ameeleza wasiwasi wake kufuatia kuwepo kwa hali ya taharuki nchini Sudan na kukariri ombi lake la kuzitaka pande zote kuweka kando misimamo mikali na maslahi ya kibinafsi, kuzingatia maslahi ya pamoja ya wananchi wa Sudan kwa kuongeza juhudi za kurejesha Serikali inayoongozwa na raia.
Katika taarifa yake iliyotolewa kutoka Geneva nchini Uswisi, Türk amekariri aliyoyasema wakati wa ziara yake nchini Sudan mwezi wa Novemba, 2022 kwamba “nchi iko katika makutano ya kufikia mwafaka. Kazi kubwa imeshafanyika na hatua nyingi chanya zimechukuliwa katika kuelekea upande wa kusaini makubaliano ya mwisho, hivyo kwa sasa lazima kufanyike juhudi zote ili kurejesha mageuzi ya kisiasa kwenye njia sahihi.”
Mwezi Desemba mwaka jana, Makubaliano ya Mfumo wa Kisiasa yalitiwa saini kati ya viongozi wa kiraia na wanajeshi nchini Sudan, kama hatua ya kwanza kuelekea kwenye kurejesha Serikali ya kiraia nchini humo.
Makubaliano ya mwisho ya kisiasa yalitarajiwa kutiwa saini tarehe 1 Aprili, 2023 lakini yaliahirishwa hadi tarehe 6 Aprili, huku ukosefu wa maelewano ukiendelea kuhusu mageuzi muhimu ya usalama na kijeshi.
Nikutokana na hali hii indio maana Kamishna Mkuu amezitaka pande zote kufanya kazi pamoja na kuepuka ucheleweshaji wowote wa kutiwa saini kwa makubaliano ya kisiasa kwani unaweza kuibua vurugu.
Amesema Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan itaendelea kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo, na kuimarisha uungwaji mkono kwa Serikali inayokuja ya kiraia.
Mkuu wa Baraza Kuu la Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan Wadau na asasi mbalimbali za kiraia nchini Sudan zimekosoa vikali kucheleweshwa utiaji saini wa makubaliano ya kurejesha amani nchini humo.
Hata hivyo Mkuu wa Baraza Kuu la Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, na wawakilishi wa mirengo mbalimbali ya kisiasa ya Sudan wanasema kwamba, kuna baadhi ya masuala ambayo bado pande mbili hazijafikia mwafaka.
Mkuu wa Baraza la Utawala na Kamanda wa Jeshi la Sudan, amesema kuwa pande husika sasa zinafanya kazi kwa bidii ili kukamilisha mjadala wa masuala yaliyosalia ili kufikia makubaliano ya mwisho ya kisiasa.
Sudan imekuwa bila serikali ya kiraia tangu Oktoba 2021 wakati jeshi lilipofuta serikali ya mpito ya Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok, na kutangaza hali ya hatari, hatua iliyopingwa na vyama vya kisiasa ambavyo viliitaja kuwa "mapinduzi ya kijeshi."