Wanafunzi kumi wa shule ya upili, Sekondari ya Umma ya Awon ya Jimbo la Kaduna lililopo kaskazini magharibi nchini Nigeria, wametekwa nyara na hawajulikani walipo tangu Aprili 3, 2023 tukio ambalo limetokea katika eneo hilo lenye visa vingi vya utekaji nyara kwa wanafunzi kwa miaka iliyopita.
Kamishna wa Usalama wa Ndani wa Jimbo la Kaduna, Samuel Aruwan amesema Wanafunzi hao, wanadaiwa kutekwa nyara katika mazingira tatanishi, huku akidai kuwa tukio hilo ni la kwanza kwa mkoa huo, tangu serikali kuanza kusambaza noti mpya, ili kukomesha malipo ya fidia kwa watekaji nyara.
Amesema, “Serikali ya Jimbo la Kaduna imepokea ripoti za awali kutoka kwa vyombo vya usalama juu ya kutekwa kwa wanafunzi karibu kumi,” Aruwan amesema katika taarifa. Haijajulikana ikiwa wanafunzi wametekwa nyara kutoka shuleni au njiani wakienda shuleni, ameongeza. “Ripoti za kina zinazotarajiwa zitaelezea.”
Kaduna ni moja ya majimbo yanayokabiliwa na magenge ya watu wenye silaha ambao hushambulia vijiji, kuuwa raia na kujihusisha na utekaji nyara ili kupata fidia ambapo katika miaka miwili iliyopita (2021/2022), mamia ya wanafunzi walitekwa nyara shuleni.