Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasauzi watia mkono, kuibeba Yanga Jumapili

98101 Wasauzi+pic Wasauzi watia mkono, kuibeba Yanga Jumapili

Fri, 6 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

KAMA bado huamini kwamba teknolojia imeimeza dunia, sikiliza Kocha wa Yanga,Luc Eymael alichofanya kuelekea mechi dhidi ya Simba Jumapili jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Eymael ameipa kazi kampuni moja ya Afrika Kusini kumchezea mechi yote dhidi ya Simba na kumpa mbinu za kuwadhibiti kila idara. Kampuni za aina hiyo hutumiwa na makocha mbalimbali wa klabu kubwa za Afrika kujua ubora hata wa wachezaji kabla ya kuwasajili.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zilizonaswa na Mwanaspoti na kuthibitishwa na Eymael mwenyewe, zinasema kwamba kazi kubwa ya kampuni hiyo ni kutumia mifumo ya kielektroniki kuirahisishia Yanga kazi.

INAFANYAJE?

Yanga imewatumia video kadhaa za Simba ambazo wanazifanyia kazi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektroniki ambayo ina uwezo wa kutoa ubora wa mchezaji mmojammoja, madhara yake uwanjani na jinsi ya kumkabili.

Eymael amekiri kwamba majibu hayo yatamuongezea mbinu za kuwapa wachezaji wake na akasisitiza kwamba vitu kama hivyo ni kawaida Ulaya wala haimaniishi kwamba kocha au benchi la ufundi limezidiwa nguvu au ujuzi, ila Afrika vilichelewa au havifahamiki sana.

Pia Soma

Advertisement
“Miongoni ya mbinu ambayo nitaitumia katika kuwakabili Simba kuna kampuni ya kuchambua wapinzani ambao nakwenda kukutana nao, ipo Afrika Kusini kama ambavyo nimefanya dhidi ya timu nyingine hivyohivyo nitafanya dhidi ya Simba ili kupata mambo ambayo nitakuwa nahitaji.

“Kampuni hiyo imekuwa ikinipatia ubora wa aina ya wapinzani kuanzia jinsi wanavyoshambulia na hata wakiwa wanashambuliwa na mambo mengine mengi ya kimbinu ambayo yatakuwa silaha kwangu ili kuwapatia wachezaji wangu, na wakati huohuo nitaongeza mbinu zangu binafsi ili kwenda kuwadhibiti wapinzani na kuwazidi,” alisema Eymael na kugoma kuweka wazi jina la kampuni hiyo.

“Ukiangalia kwa uwezo wa mchezaji mmojammoja Simba wanaonekana kama kutuzidi, lakini ukweli ulivyo katika mechi hizi kubwa mara nyingi jambo hilo halipo, bali timu ambayo inacheza kwa pamoja kwa maana ya kushambulia na kukaba tena ikiwa na nidhamu kubwa hiyo ndio inafanikiwa.

“Kwa maana hiyo katika siku hizi chache naandaa timu ambayo itakwenda kucheza kwa pamoja na mbinu nyingi zaidi kuliko kucheza kila mchezaji kwa uwezo wake, jambo ambalo nina imani nitafanikiwa na kwenda kupata matokeo mazuri kwa upande wetu.”

Eymael alisema: “Kulingana na ukubwa wa mechi hii ndio maana nilianza maandalizi mapema kwani hata katika mchezo wetu na Mbao nilipumzisha baadhi ya wachezaji kama Bernard Morrison, Said Juma, Jaffary Mohammed na wengineo ili kukwepa kupata majeraha na wengine kadi ambazo zingewafanya kukosa mechi na Simba.

“Kwa maandalizi ambayo tutaendelea kuyafanya mpaka siku ya mechi naona timu yangu itakuwa na nafasi kubwa ya kuonyesha ubora katika maeneo mengi kulingana na mbinu ambazo nimeendelea kuwapatia tofauti kabisa na wakati nilivyoikuta timu inacheza.”

HATA AUSSEMS ALIITUMIA

Mwanaspoti linafahamu kampuni hiyo ambayo anaitumia Eymael katika kuichambua Simba, Kocha wa zamani wa Mnyama, Patrick Aussems naye alikuwa akiitumia hata wakati wa usajili wa dirisha kubwa msimu huu waliitumia pia, ndio wakawapata wachezaji kadhaa akiwemo Deo Kanda naTairone Santos.

Kampuni hiyo imetumiwa na timu nyingi kubwa za soka hapa Afrika kama Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ilipotaka kumsajili kiungo James Kotei kutoka Simba.

Jina la Kotei lilipelekwa na video zake wakazifanyia kazi fasta Simba wakaja kushtuliwa dakika za mwisho lakini wakalazimika kumuachia tu aende akakipige katika klabu hiyo ya Bondeni.

Chanzo: mwananchi.co.tz