Takriban wagombea wote wa upinzani katika uchaguzi mdogo wa Zimbabwe uliopangwa kufanyika Jumamosi, ambao unaweza kufungua njia ya kupatikana kwa thuluthi mbili ya wabunge katika Bunge la chama tawala, walizuiwa kuwania na mahakama siku ya Alhamisi.
Mahakama ya Harare iliamuru, katika uamuzi ambao shirika la habari la AFP limepata na nakala yake, kwamba wawakilishi 8 kati ya 9 wa chama cha kwanza cha upinzani, Chama cha Wananchi (CCC), "sio wagombea katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika tarehe 9 Desemba. " na kwamba majina yao "hayajajumuishwa kwenye kura".
Uamuzi huu unakuja katika hali ya mvutano wa kisiasa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, huku upinzani ukilaani mara kwa mara ukandamizaji wa kikatili unaofanywa na serikali, kupitia kuwakamata wapinzani na utekaji nyara unaoambatana na vitendo vya utesaji. CCC tayari imeonyesha kuwa imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama uliotangazwa siku mbili kabla ya uchaguzi: "Mahakama ya Zimbabwe imekoma kuwa mwamuzi wa haki na isiyoegemea upande wowote," amelaani msemaji wa chama Promise Mkwananzi.
Raia wa Zimbabwe wanatarajiwa kupiga kura siku ya Jumamosi. Nchi hiyo ilifanya uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mwezi Agosti, ambao ulipelekea kuchaguliwa tena kwa Rais Emmerson Mnangagwa, 81, na kupewa viti 177 kati ya 280 vya Bunge kwa chama chake, Zanu-P, madarakani tangu uhuru mwaka 1980.
Mnamo Oktoba, Wabunge 14 wa CCC walipoteza viti vyao baada ya njama iliyofaulu ya mtu aliyetajwa na CCC kama "mdanganyifu", hali ambayo ilisababisha kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika maeneo 9 ya uchaguzi. Sengezo Tshabangu, akijionyesha kama "Kaimu Katibu Mkuu" wa CCC, alitangaza katika barua aliyoiandikia Bunge kuwa wabunge husika wamekihama chama.
Kiongozi wa CCC, Nelson Chamisa, alimwomba spika wa Bunge hilo kupuuzia mbali barua hiyo, akithibitisha kwamba chama hicho hakina katibu mkuu na kwamba hajamfukuza wala kumsimamisha mbunge yeyote ule. Lakini Bunge hata hivyo lilitangaza viti vilivyokuwa wazi kwa tume ya uchaguzi. Sengezo Tshabangu alichukua hatua za kisheria kuwataka wabunge waliofukuzwa wasiweze kusimama tena katika uchaguzi mdogo wa Jumamosi.
Akihojiwa na shirika la AFP, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Rodney Kiwa, alitangaza kwamba italazimika "kuzingatia" uamuzi wa hivi punde wa mahakama. Zanu-PF inahitaji tu viti 10 zaidi ili kupata thuluthi mbili ya wabunge katika Bunge na kuweza kurekebisha Katiba kwa uhuru.