Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanigeria wajificha vichakani kwa kuhofia kutekwa nyara

Wanigeria Wajificha Vichakani Kwa Kuhofia Kutekwa Nyara Wanigeria wajificha vichakani kwa kuhofia kutekwa nyara

Tue, 28 May 2024 Chanzo: bbc

Walionusurika katika tukio la hivi punde la utekaji nyara wa watu wengi kaskazini mwa Nigeria wameiambia BBC kwamba wanahofia maisha yao.

Takriban watu kumi waliuawa na wengine 160, wengi wao wanawake na watoto, walitekwa nyara Ijumaa iliyopita katika kijiji cha Kuchi katika jimbo la Niger.

Mkazi mmoja aliiambia BBC kwamba watu sasa wanajificha vichakani, baada ya wavamizi wengine kurejea Jumapili usiku.

Mke wa Jubril alikuwa akirudi kutoka kwa nyumba ya babake Ijumaa jioni alipotekwa.

"Nina huzuni. Inasikitisha sana. Wakati wowote wanaweza kurudi. Watu waliobaki wanajaribu kujificha vichakani.” Kamishna wa Usalama wa Ndani wa Jimbo la Niger, Muhammed Bello, alisema idara yake, pamoja na "vyombo mbalimbali vya usalama", vinachunguza utekaji nyara huo, ingawa amepinga idadi ya watu waliochukuliwa.

"Kwa kweli haimaanishi kwamba wote wamechukuliwa na waasi au majambazi, baadhi yao huenda wamekimbilia msituni au kuvuka maji kwa sababu ya mkanganyiko." Kamishna huyo alisema serikali inafanyia kazi mpango wa mashirika mbalimbali ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya mashambulizi. Tunashirikiana kwa hivyo tuna operesheni hizi za kijeshi zinazofanyika katika majimbo kwa wakati mmoja, kwa hivyo hakutakuwa na njia ya kutoroka kwa yeyote kati yao." Hata hivyo, wakosoaji wanaishtumu serikali kwa kushindwakuzuia mashambulizi, ambayo yamekithiri katika majimbo ya kaskazini. Akiongea kwa niaba ya mgombea urais wa chama cha Labour Peter Obi, Dkt Yunusa Tanko aliiambia BBC kuwa ongezeko la idadi ya utekaji nyara katika maeneo fulani "si la kushangaza", kwa sababu ya kile alichoeleza kuwa kupuuzwa kwa serikali za mitaa katika maeneo ya mashambani. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema "lina wasiwasi mkubwa" juu ya utekaji nyara wa watu wengi, likisema "ni dalili nyingine ya kushindwa kabisa kwa mamlaka ya Nigeria kulinda maisha." Katika kipindi cha mwezi uliopita, vijiji kadhaa vimevamiwa na magenge yenye silaha ambayo yanawateka nyara ili kujipatia fidia. Mara nyingi haijulikani ikiwa watu hao wenye silaha wana uhusiano wowote na makundi ya kijihadi.

Chanzo: bbc