Wanawake 11 wa Burundi wameondoka kwenye uwanja wa ndege wa Bujumbura na kuelekea Saudi Arabia kufanya kazi za nyumbani katika mpango wa serikali zote mbili zinazounga mkono mpango wa kuzuia uhamiaji haramu wa wafanyikazi.
Mamia ya wanawake wa Burundi, wengi wao wakiwa wasichana wadogo, wamesafirishwa na makampuni ya biashara kwenda kufanya kazi za nyumbani katika nchi za Kiarabu, na baadhi yao wamesema kuwa walivumilia ukatili wa nyumbani uliokithiri.
"Nina furaha sana…baada ya takriban miaka minne ya kukosa kazi", Aline Niyokwizera, 22, kutoka kusini mwa Burundi aliambia BBC katika uwanja wa ndege wa Bujumbura muda mfupi kabla kuwajaondoka.
Sitini kati yao, wote wakiwa wamevalia mavazi ya wanawake wa Kiislamu, walikuwa kwenye uwanja wa ndege tayari kuondoka lakini kumi na moja pekee ndio waliokwenda, waliosalia watasafiri siku ya Ijumaa baada ya kukosa viti kwenye ndege ya Jumatano jioni.
Jean Bosco Bizuru kiongozi wa wakala wa kuajiri wafanya kazi wa ndani alisema wamewafunza wanawake kazi za nyumbani ambazo watakuwa wakifanya nchini Saudi Arabia.
Burundi inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, ambao ni zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo.
Epimeni Bapfinda, afisa katika wizara ya mashauri ya nchi za kigeni alisema zaidi ya nafasi za kazi 75,000 kwa Warundi zitapatikana nchini Saudi Arabia.