SUDAN Kusini imeanza kuondoa ada za visa kwa raia wa kigeni wanaokimbia vita katika mpaka wake na nchi jirani ya Sudan kuanzia wiki hii.
Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi ya Usajili wa Raia, Pasipoti na Uhamiaji, Atem Marol Biar amewaagiza maofisa wa uhamiaji katika vituo vyote vya kuvuka mpaka na Sudan kutotoza ada za viza kwa wageni.
“Kuhusu suala la watu wanaotoka Sudan, tumetoa maelekezo ya wazi kwa mujibu wa sheria ya kimataifa. Watu wanaokimbia mzozo wanapaswa kupokelewa vyema na nimeelekeza maofisa kuwaruhusu bila kuomba malipo ya viza,” alisema Biar.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, wageni watakaoamua kukaa nchini kama wakimbizi watasajiliwa na mamlaka kwa kushirikiana na mashirika ya kibinadamu.