Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wajawa nyongo kupanda gharama za maisha Nigeria

Nigeria Nigeroiaaaa Wananchi wajawa nyongo kupanda gharama za maisha Nigeria

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Raia wa Nigeria wanakabiliwa na uhaba wa mafuta ya petroli na hali ya mchafukoge katika mabenki katika jitihaa za kubadilishana sarafu za zamani na mpya kabla ya uchaguzi wa rais baadaye mwezi huu.

Foleni ndefu za magari na vyombo vingine vya moto zimekuwa zikishuhudiwa katika miji mbalimbali ya Nigeria kwa masaa kadhaa kwa ajili ya kupata huduma ya mafuta ya petroli huku misururu ya watu ikishuhudiwa katika mabenki na vituo vya ATM kwa ajili ya kubadilisha sarafu zao za zamani na kupata mpya.

Ripoti zinasema, kuanzia maeneo ya kaskazini hadi kusini, nchi ya Nigeria yenye idadi ya watu wapatao milioni 215 inakabiliwa na mchanganyiko tata wa matatizo yanayojumuisha uhaba wa mafuta ya petroli, mparaganyiko na hali ya mchafukoge katika mabenki kuhusu mchakato wa kupata sarafu mpya, pamoja na ukosefu wa maji na umeme.

Nigeria ambayo ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ghafi barani Afrika, ina mitambo ya kizamani ya kusafisha bidhaa hiyo na uwezo mdogo wa kusafisha mafuta, hivyo inalazimika kuagiza mafuta kutoka Ulaya na kwingineko ili kupunguza foleni kubwa za raia wanaohitaji huduma hiyo. Wagombea kiti cha rais katika uchaguzi wa Nigeria

Wakati huo huo misururu ya watu imeonekana ikikusanyika nje ya mabenki, na watu zaidi wakiendelea kujiunga na umati.

Wanaigeria wanajaribu kupata noti mpya zilizozinduliwa Oktoba mwaka jana kuchukua nafasi ya Naira ya zamani, na tarehe ya mwisho ya kubadilishana noti mpya na za zamani ilikuwa Januari 31.

Hata hivyo siku chache kabla ya tarehe ya mwisho, ni benki chache tu ndizo zilizokuwa zikisambaza noti mpya, na kuwaacha Wanigeria wengi ambao ni masikini wa kupindukia na hawana akaunti za benki, bila kupata pesa mpya.

Serikali ya Nigeria imelazimika kurefusha tarehe ya mwisho ya zoezi hilo hadi Februari 10 lakini hadi Jumanne wiki hii benki nyingi hazikuweza kusambaza noti mpya.

Wagombea wawili wakuu wanaowania kuchukua nafasi ya Muhammadu Buhari ni Bola Tinubu wa chama tawala cha rais wa sasa na Atiku Abubakar wa kundi kuu la upinzani.

Wawili hao ni wanasiasa wakongwe na matajiri lakini pia wanaandamwa na tuhuma za ufisadi.

Uchaguzi wa rais wa Nigeria wa 2023 utafanyika tarehe 25 Februari 2023 kumchagua rais na makamu wa rais wa Nigeria. Chaguzi zingine za shirikisho, ikiwa ni pamoja na chaguzi za Baraza la Wawakilishi na Seneti, pia zitafanyika tarehe hiyo hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live