Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameliambia jeshi la Uganda (UPDF} kuwahusisha raia katika juhudi zao kuwasaka wanamgambo wa kundi la kigaidi la {Allied Democratic Force) – ADF.
Wiki iliyopita wanamgambo hao walifanya mashambulizi katika mbuga ya kitaifa nchini humo ya Malkia Elizabeth ambapo raria wawili wa kigeni na mmoja wa Uganda waliuawa.
Rais huyo aliyenukuliwa na vyombo vya Habari nchini humo alipotoa taarifa kwa taifa Jumapili, amesema kwamba shughuli za kuwasaka watu hao waliotelekeza shambulizi hilo bado linaendelea akiongeza kuwa msako pia unawalenga walioteketeza moto lori moja mjini Kasese.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X -zamani ikiitwa Twitter, Rais Museveni anasisitiza kwamba, ‘UPDF inapaswa kuihusisha idara ya polisi, na raia (wananchi) kusaka haya makundi yanayotokea Congo ,’
‘‘Watu hawa sio tatizo la jeshi pekee yake, Ni jukumu la vitengo mbali mbali vya usalama kama polisi, idara ya uhjasusi na kila mmoja wetu kuhakikisha vita dhidi ya ugaidi vinafaulu, ‘ aliogeza Rais Museveni.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, jeshi la UPDF lilitekeleza ushambulizi katika kambi ya kundi la kigaidi la ADF katika eneo la magharibi mwa DRC ambapo jeshi la Uganda linasema kambi kuu ya ADF ililengwa na kuharibiwa.