Wakati huu wananchi wa Zimbabwe, wakiiendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi wa urais, uliofanyika siku ya Jumatano na kuendelea mpaka jana, polisi wanasema wamewakamata waangalizi 41 wa ndani.
Waangalizi hao kutoka vuguvugu la kupigania demokrasia, walikamatwa Jumatano usiku jijini Harare na vifaa vyao vya kazi kama tarakilishi na simu kuchukuliwa.
Polisi wanasema, wamechukua hatua hiyo kwa madai kuwa waangalizi hao walikuwa wanajumuisha matokeo ya urais, kitendo ambacho wanasema ni kinyume cha sheria.
Hatua hii imekuja, wakati huu upinzani ukidai mbinu chafu za kuiba kura, baada ya upigaji kura kucheleweshwa katika ngome zao, kwa lengo la kuwakatisha tamaa wapiga kura.
Rais Mnangagwa anatazamiwa kupata ushindi na hivyo kumuwezesha kuendelea kuingoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa muhula wa pili na wa mwisho katika nchi yenye utajiri wa maliasili. Wagombea wakuu wawili wa kiti cha urais Zimbabwe Nelson Chamisa (kushoto) na Rais Emerson Mnangagwa anayetetea kiti chake
Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 80, alichukua wadhifa huo wakati kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe alipoondolewa katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2017. Rais Mnangagwa anachuana na wagombea wengine 10, akiwemo mpinzani wake mkuu, wakili na mchungaji Nelson Chamisa, 45, wa Chama cha Citizens Coalition for Change.
Katika uchaguzi huu Wazimbabwe walichagua madiwani na wabunge wapya lakini kinyang'anyiro cha urais ni muhimu zaidi.
Uchaguzi huu pia utaamua muundo mpya wa bunge lenye viti 350 na zaidi ya nyadhifa 1,900 za udiwani.
Baadhi ya wapiga kura walisubiri zoezi hilo kwa saa nyingi, wakisema walikuwa na matumaini ya mabadiliko ya kiuchumi, lakini wachambuzi wamekuwa na shaka, iwapo chama tawala cha ZANU-PF, kitaruhusu uchaguzi huru kufanyika au kuachia madaraka.
Mgombea wa chama kikuu cha upinzani katika uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa amedai kuwa zoezi la upigaji kura la jana limekumbwa na kasoro nyingi na udanganyifu mkubwa, na kwamba kuna njama za kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo.