Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanamuziki wanavyotumika kwenye kampeni Uchaguzi DRC

Tsheskedi Papa Mopao.jpeg Wanamuziki wanavyotumika kwenye kampeni Uchaguzi DRC

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kinshasa. Wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikitarajia kufanya uchaguzi Jumatano Desemba 20, 2023, baadhi ya wanamuziki nchini humo wametunga nyimbo za kampeni zinazomuunga mkono Rais Felix Tshisekedi, anayewania muhula wake wa pili.

Limekuwa ni jambo la kawaida kwa wanamuziki wengi wa DRC kumuunga mkono Rais aliyepo madarakani, ilikuwa hivyo tangu wakati wa Rais Joseph Kabila na sasa kwa Tshisekedi, jambo ambalo limewafanya wanamuziki hao kuchukiwa na raia wa DRC wanaoishi nje Ulaya na Marekani na kuwafanya wazuie matamasha yao kwenye nchi wanazotembelea.

Inaelezwa wanamuziki hao wanalipwa vizuri na wagombea hao, jambo ambalo linawavutia wengi kuingia kwenye mkumbo huo wa kuwafanyia kampeni watawala hao.

Baadhi ya wasanii wakubwa ambao tayari wamerekodi nyimbo maalumu kwa ajili ya kumuunga mkono Tshisekedi ni pamoja na Koffi Olomide, JB Mpiana, Werrason na Blaise Bula.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limefanya mahojiano na Bula ambaye ameeleza hajalipwa kurekodi wimbo wa kumuunga mkono Tshisekedi, bali amevutiwa na kazi kubwa aliyoifanya kwenye muhula wake wa kwanza hususani kutoa elimu ya msingi kwa wote bila malipo.

Hata hivyo, msanii wa kizazi kipya wa DRC anayeishi Ulaya, Bob Elvis amesema hawezi kumuunga mkono kiongozi ambaye hamwamini.

"Hakuna kiasi cha pesa ambacho kinaweza kunishawishi kuunga mkono mambo ambayo siamini," rapa Elvis amenukuliwa na BBC.

Kwa upande mwingine, nyota anayechipukia, Infrapa amewataka mamia kwa maelfu ya wafuasi wake wa Facebook kumpigia kura mfanyabiashara tajiri na mmoja wa wapinzani wakubwa wa Rais Tshisekedi, Moise Katumbi katika uchaguzi Jumatano ijayo.

Mwenendo huo wa wasanii kuwaunga mkono wagombea, si DRC pekee. Umekuwa hivyo pia katika nchi za Afrika Mashariki. Hata hivyo, wapo wasanii wenye misimamo tofauti, wakikataa kujihusisha na wagombea urais na siasa zao.

Wasanii wa Tanzania, Alikiba na Diamond pia walialikwa kutumbuiza kwenye kampeni hizo kama moja ya silaha za wanasiasa kuongeza mvuto na ushawishi kwenye mikutano yao kabla ya uchaguzi wenyewe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live