Maafisa wa usalama wa Burkina Faso wamesema Jumanne kwamba darzeni ya wanajeshi pamoja na wapiganaji wa kujitolea wameuwawa kwenye shambulizi linaloshukiwa kutekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi.
Ikiwa moja ya nchi masikini zaidi duniani, Burkina Faso inakabiliana na wanamgambo wa kijihadi walioanza kwenye nchi jirani ya Mali 2015. Takriban thuluthi mbili za taifa hilo zipo nje ya udhibiti wa serikali kulingana na serikali, suala lililopelekea kubuniwa kwa kikosi cha watu wa kujitolea cha Volunteers for the Defence of the Fatherland, ambao hupewa mafunzo ya kijeshi ya wiki mbili kabla ya kujiunga kwenye operesheni.
Kwa kawaida kikosi hicho hufanya kazi pamoja na jeshi kwenye nyanja za uangalizi, ukusanyaji wa taarifa pamoja na kusindikiza wasafiriw. Shambulizi la jana dhidi ya kijiji cha Noaka kati- kaskazini mwa nchi linasemekana kulenga watu kutoka kikosi cha VDP, huku kundi lingine la washambuliaji likilenga wanajeshi waliokuwa wakirejea baada ya kusindikiza wasafiri kwenye eneo la Sahel.