Rais wa Kenya, William Ruto anatarajia kuaga kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), kinachoelekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), eneo ambalo mapigano makali yanaendelea kati ya jeshi na kundi la wapiganaji wa M23.
Vikosi hivyo vya Kenya, vitajiunga na kikosi cha kanda kitakachosaidia kupambana na makundi yenye silaha, huku Jeshi la DRC likipambana na pande zinazopigana za kundi la Islamic State – Allied Democratic Forces ADF, na makundi mengine kadhaa yenye silaha.
Wazo la kutuma jeshi la kikanda lilitolewa na kuidhinishwa mwezi Juni, wakati Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta (Mjumbe wa amani wa Kenya), alipoitisha mkutano wa amani wa viongozi wa Jumuiya ya Africa ya Mashariki EAC.
Kenya ilichaguliwa kuongoza juhudi za kidiplomasia na kijeshi na hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa EAC kutuma wanajeshi katika nchi wanachama.