Idadi isiyojulikana ya wanajeshi wa Kenya wanahofiwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi (IED) katika kaunti ya Lamu pwani siku ya Jumapili.
Msemaji wa jeshi Brig Zipporah Kioko aliambia tovuti ya Nation kuwa kisa hicho kilitokea katika msitu wa Boni kaunti ya Lamu.
Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika taarifa siku ya Jumatatu lilisema wanajeshi hao walikuwa wakishika doria kando ya barabara ya Milimani Baure wakati kisa hicho kilipotokea.
"Waliojeruhiwa walisafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Manda Base kwa matibabu," ilisema taarifa ya KDF.Taarifa hiyo haikutaja idadi ya wanajeshi waliouawa.
Kundi la wanamgambo wa Al-Shabab limesema lilitekeleza shambulio hilo.
Wanamgambo hao wa Somalia wameongeza mashambulizi Lamu katika wiki za hivi karibuni, mara nyingi wakilenga vikosi vya usalama.
Kuongezeka kwa mashambulizi kumeilazimu serikali kusitisha mpango wa kufungua tena mpaka wa Kenya na Somalia.