Wanajeshi saba wa DR Congo wamehukumiwa kifo kwa kuonyesha uoga mbele ya wapiganaji wa kikundi cha waasi wa M23 na kukimbia hali inayodaiwa kuzidisha hofu kwa wananchi.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi alisema tarehe 9 Februari 2023, wanajeshi hao walipitia katikati ya eneo la Sake, kilomita 25 magharibi mwa mji wa Goma uliopo mashariki mwa Kongo, wakipiga risasi kiholela walipokuwa wakiwakimbia waasi hao.
Hata hivyo, wanajeshi hao walikanusha mashtaka na mawakili wao walisema watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo.
Mwendesha mashtaka alisema raia wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya wakati wa tukio hilo lililosababishwa na kitendo cha askari.
Maelfu ya watu hivi karibuni wamekimbia makazi yao hadi Goma na Minova huku waasi wa M23 wakikaribia mji huo kutoka eneo la Masisi magharibi.
Novemba mwaka jana, mahakama ya kijeshi ya Goma iliwahukumu kifo askari watatu kwa kukimbia vitani wakati wa makabiliano dhidi ya M23 na kusababisha hofu miongoni mwa raia.
Adhabu za kifo bado zinatolewa nchini DR Congo lakini mara ya mwisho zilitekelezwa mwaka 2003. Aidha, adhabu hizo zimeanza kubadilishwa taratibu na kuwa kifungo cha maisha.